Okwi atoa sababu iliyowamaliza Simba

27Jan 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Okwi atoa sababu iliyowamaliza Simba

BAADA ya kushindwa kutinga fainali ya mashindano ya Kombe la SportPesa, mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema wachezaji wa timu hiyo akili na mawazo yao wameyaweka zaidi kufikiria michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

EMMANUEL OKWI

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanaofundishwa na Mbelgiji Patrick Aussems, watasafiri kuifuata Al Ahly katika mchezo wake wa tatu wa Kundi D utakaochezwa Februari 2, mwaka huu mjini Alexandria, Misri.

 

Akizungumza na gazeti hili jana, Okwi alisema waliingia uwanjani kwa ajili ya kupambana kusaka ushindi jambo ambalo lilishindikana katika mchezo huo na kuongeza kwamba mechi zote walizocheza zilikuwa ngumu na zenye ushindani.

 

Okwi alisema kufungwa ni sehemu ya matokeo ya mchezo, lakini wao kama wachezaji wa Simba wanafahamu wana jukumu kubwa la kufanya vizuri kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

"Tulijipanga kuchukua kikombe hiki, lakini Mungu alikuwa na mipango mingine, sisi akili yetu inatizama zaidi mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi hizi za SportPesa Cup zimetusaidia kujiimarisha kuelekea mechi yetu inayokuja ambayo tutachezea Misri," alisema mshambuliaji huyo raia wa Uganda.

 

Ndoto za Simba ambayo ilicheza fainali ya SportPesa Cup mwaka juzi na mwaka jana, kuvaana na Everton inayoshiriki Ligi Kuu England imezimwa na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bandari FC ya Kenya.

 

Simba itaifuata Al Ahly huku ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 5-0 ilichokipata mjini Kinshasa, DR Congo kutoka kwa wenyeji wao AS Vita.

 

Habari Kubwa