Okwi, Bocco wang'ara TFF

14Jun 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Okwi, Bocco wang'ara TFF
  • ***Waachiwa tuzo Mchezaji Bora wa Mwaka, Nyoni naye kidedea...

NI mwaka wa Simba... hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na sasa wachezaji wa klabu hiyo wanajiandaa kupokea tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake maalum ya tuzo za Ligi Kuu, jana lilitoa majina matatu ya mwisho yatakayopigiwa kura kuwania tuzo hiyo.

Habari njema kwa Simba ni kwamba majina yote matatu yametoka kwenye kikosi hicho na hivyo kuwa na uhakika wa kutoa Mchezaji Bora wa msimu.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, wachezaji waliopitishwa kuwania tuzo hiyo ni washambuliaji Emmanuel Okwi, John Bocco na kiraka Erasto Nyoni.

Wachezaji hao wamepenya kwenye orodha ya awali ya wachezaji 30 waliokuwa wametajwa kuwania tuzo hiyo kabla ya kupitishwa mchujo na kubaki majina hayo.

Wachezaji hao watapigiwa kura na makocha na manahodha wa timu za Ligi Kuu, lakini pia wahariri wa habari za michezo.

Nyota hao, Okwi, Bocco na Nyoni hivi karibuni wametwaa tuzo ndani ya klabu hiyo.

Kama Okwi atatwaa tuzo hiyo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu, atakuwa amepiga 'hat-trick' ya tuzo kwa kuwa mbali na tuzo ya klabu, pia atakabidhiwa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ambayo tayari ana uhakika nayo.

Sherehe za utoaji tuzo hizo zimepangwa kufanyika Juni 23, mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mbali na tuzo hiyo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu, pia zitatolewa tuzo nyingine za Mchezaji Bora chini ya umri wa miaka 20 (Tuzo ya Ismail Khalfan), inayohusisha vikosi vya vijana vya timu za Ligi Kuu yenyewe inaendelea kufanyiwa kazi kwa vile mashindano yanaendelea mkoani Dodoma na itakapokamilika watatangazwa wateule watatu.

Tuzo nyingine zitakazotolewa siku hiyo ni Timu yenye Nidhamu inayowaniwa na Kagera Sugar, Simba na Mtibwa Sugar, wakati Mchezaji Bora Chipukizi inawaniwa na Shaaban Idd Chilunda, Yahya Zayd (Azam) na Habibu Kiyombo (Mbao).

Mwamuzi Msaidizi Bora inawaniwa na Helen Mduma, Mohammed Mkono na Ferdinand Chacha, wakati Mwamuzi Bora wateule ni Elly Sasii, Jonesia Rukyaa na Hans Mabena.

Tuzo ya Kipa Bora wanaowania ni Aron Kalambo (Prisons), Aishi Manula (Simba) na Razack Abalora (Azam), huku Kocha Bora wateule ni Abdallah Mohamed (Prisons), Zuberi Katwila (Mtibwa) na Pierre Lechantre (Simba).

Bao Bora ni Seif Karihe (Lipuli) na Shaaban Idd Chilunda (Azam) ambaye ameingiza mabao mawili.

Habari Kubwa