Okwi kuvuna mil. 226/- Simba

27Jun 2017
Faustine Feliciane
Dar es salaam
Nipashe
Okwi kuvuna mil. 226/- Simba
  • ***Mo asema hiyo ni zawadi ya Sikukuu ya Idd, yeye adai ni mapenzi tu na kwamba...

KLABU ya Simba imeonyesha jeuri ya fedha baada ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji raia wa Uganda, Emmanuel Okwi, ambaye ataigharimu Sh. milioni 226. 2, kwa kipindi cha miaka miwili ya mkataba wake.

Simba ambayo imemsainisha Okwi mkataba wa miaka miwili kwa gharama ya Dola za Marekani 65,000 sawa na Sh. milioni 142.2, pia imekubali kumlipa mshahara wa Sh. milioni 3.5 kwa mwezi.

Hivyo, kwa kipindi cha miaka miwili ambayo Okwi ataichezea Simba, kwa upande wa mshahara tu, atatia kibindoni Sh. milioni 84 ambazo ukijumlisha na Sh. milioni 142.2 za usajili, zinamfanya kuvuna jumla ya Sh. milioni 226. 2 kwa kipindi chake cha miaka miwili atakayoichezea Simba.

Akizungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa kuwa ndiyo utaratibu wa klabu yao waliojiwekea kwa sasa, mmoja wa kiongozi wa Simba alikiri Okwi kusaini kwa kiasi hicho cha fedha na kwamba atakuwa akilipwa Sh. milioni 3.5 kwa mwezi.

Simba kwa sasa imejiwekea utaratibu wa viongozi wake kutozungumza moja kwa moja na vyombo vya habari na badala yake taarifa zitakuwa zikipatikana katika mtandao wao.

Lakini Okwi, ambaye ametua Simba akitokea SC Villa ya Uganda, jana alisema amefurahi kurejea katika timu hiyo iliyomlea na kumtunza kabla hajaenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.

"Kwangu mimi naona kama nimerudi nyumbani na mapenzi na timu hii ndio yamenifanya nikubali kujiunga nayo tena, nashukuru sana," alisema Okwi.

Dili la nyota huyo kutua Msimbazi limesimamiwa na kuwezeshwa na mdau wa timu hiyo, mfanyabiashara Mohamed Dewji maarufu kwa jina la Mo.

Dewji, jana alionekana kwenye mitandao mbalimbali katika video fupi akiwa na mshambuliaji huyo, akisema amemleta nchini mchezaji huyo kama zawadi ya Sikukuu ya Idd kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.

Mara ya mwisho Okwi kuichezea Simba ilikuwa mwaka 2015, kabla ya klabu hiyo kumuuza klabu ya Sonderjyske ya Denmark ambako alijiunga nayo kwa mkataba wa miaka mitano.

Hata hivyo, Okwi hakudumu kwenye timu baada ya kuvunja mkataba kwa makubaliano ya pande zote mbili na kurejea kwao Uganda na kujiunga na SC Villa.

Habari Kubwa