Okwi: Mbelgiji ameleta vita

05Aug 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Okwi: Mbelgiji ameleta vita
  • ***Aidha, Simba itarejea leo huku Asante Kotoko wakitua nchini Jumanne tayari...

WAKATI Asante Kotoko ikitarajiwa kutua keshokutwa Jumanne tayari kuivaa Simba ambayo inarejea nchini leo, mshambuliaji wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, Emmanuel Okwi,-

amesema kikosi chao kimeiva na kiko tayari kuanza kupambana kutetea ubingwa huo wanaoushikilia kwa kuwa kocha mpya Mbelgiji, Patrick Aussems, ameamsha changamoto mpya.

 

Akizungumza na gazeti hili jana, Okwi alisema wakiwa Uturuki wamefanya mazoezi magumu ambayo yamewajenga na kuwaweka tayari kukabiliana na changamoto za ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Agosti 22, mwaka huu.

Okwi alisema ujio wa kocha Mbelgiji Aussems, pia umesaidia "kuwaamsha" wachezaji kwa sababu kila mmoja anataka kumuonyesha ana uwezo ili apate namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Alisema mbali na kujipanga kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara, pia wanataka kuona wanafika mbali kwenye mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo watashiriki baadaye mwaka huu.

"Naweza kusema tuko tayari kuanza ligi au mashindano yoyote, tumefanya vizuri katika kambi yetu na naamini benchi la ufundi limetimiza programu ambayo waliiandaa katika muda wote tuliokuwa huku [Uturuki]," alisema mshambuliaji huyo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara, alisema jana kuwa kikosi cha timu yao kinatarajia kurejea nchini leo alfajiri na kikiwa tayari kushiriki katika Tamasha la Simba Day litakalofanyika Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa.

Manara alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na wageni wao Asante Kotoko kutoka Ghana wanatarajia kuwasili nchini Jumanne.

"Mipango na program zetu kuelekea wiki ya Simba Day zinaendelea vema na tunatarajia kuwapokea vijana wetu kesho (leo) alfajiri huku mgeni Asante Kotoko  atakuwa katika ardhi ya Tanzania Jumanne," Manara alisema.

Simba leo inatarajia kutambulisha jezi mpya ambazo watazitumia katika msimu mpya pamoja na bidhaa mbalimbali zenye nembo ya klabu hiyo yenye makao makuu yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa