Okwi moto, aiweka Uganda njia moja

01Sep 2017
Na Mwandishi Wetu
Kampala
Nipashe
Okwi moto, aiweka Uganda njia moja
  • ***Bao lake laiua Misri na kuifanya Uganda iendelee kuongoza katika kundi ....

MSHAMBULIAJI wa Simba, Emmanuel Okwi, aliifungia timu yake ya Taifa ya Uganda (Cranes) bao pekee dhidi ya Misri "Mafarao" katika mechi ya kuwania tiketi ya kufuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Namboole jijini hapa.

Ushindi huo wa jana uliifanya Uganda iendelee kuongoza katika Kundi E baada ya kufikisha pointi tisa ikifuatiwa na Misri wenye pointi saba na Ghana yenye pointi moja huku Congo Brazzaville ambao hawana pointi hata moja wakiburuza mkia.

Okwi ambaye alikuwa mwiba katika mechi hiyo alipachika bao hilo katika dakika ya 51 huku pia akiwa mwimba kwa Misri kwa kufanya mashambulizi kadhaa kwenye mchezo huo uliokuwa na kasi.

Uganda ambayo sasa iko chini ya kocha wa zamani wa Simba, Moses Basena inatarajia kusafiri kuifuata Misri katika mechi ya marudiano itakayofanyika Jumanne jijini Alexandria.

Mara ya mwisho Uganda kuifunga Misri ilikuwa ni 1965.

Bao hilo la Okwi alilofunga jana, ni goli la tano ndani ya siku sita baada ya Jumamosi iliyopita kufunga manne wakati Simba ikiibuka na ushindi wa magoli 7-0.

Kutokana na majukumu hayo, Okwi na beki wa kati wa Simba, Juuko Murshid wataukosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu yao dhidi ya Azam FC utakaofanyika Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Simba katika kuendelea kusaka makali kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC itakayofanyika Jumatano, leo itawakaribisha Hard Rock kutoka Zanzibar katika mechi ya kirafiki itakayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara, alisema jana kuwa Kocha Mkuu Joseph Omog anatarajia kuitumia mechi hiyo kuwaweka tayari baadhi ya nyota wake ambao hawakupata nafasi ya kucheza kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na ile ya ufunguzi waliyoipa kichapo cha mabao 7-0 Ruvu Shooting.

Manara alisema kuwa wanaamini mchezo huo wa kirafiki utasaidia kuendeleza kasi na "spidi" walioianza msimu huu wakati wakiipisha timu ya Taifa (Taifa Stars) kupeperusha bendera ya nchi.