Omog afuata tatu za Prisons

14Nov 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Omog afuata tatu za Prisons
  • ***Lengo la Maafande hao kuwafuta mashabiki machozi Mbeya lamtisha...

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema kikosi chake kimerejea Mbeya salama kwa ajili ya kumalizia kazi iliyobakia ya kubeba pointi tatu nyingine muhimu dhidi ya Tanzania Prisons ya jijini humo.

Maafande hao ambao walienda kuweka kambi mkoani Njombe, wanatarajiwa kuikaribisha Simba katika mechi ya raundi ya 10 ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Omog, ambaye timu yake hiyo inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, alisema kuwa anafahamu mechi hiyo ya Jumamosi itakuwa ngumu kuliko iliyopita dhidi ya Mbeya City kwa sababu wachezaji wa Prisons wanahitaji kuwafuta "machozi" mashabiki wao kwa kupata matokeo mazuri.

Omog amewakumbusha wachezaji wake kuwaheshimu wapinzani wao na kuongeza umakini katika dakika zote 90 za mchezo huo.

"Najua utakuwa mchezo mgumu kama mechi nyingine, ila tunataka kupambana ili kukamilisha kazi ya kupata pointi zote sita katika mkoa wa Mbeya, si kazi rahisi, lakini ninaamini tunaweza," alisema kocha huyo wa zamani wa Azam FC ya Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa mechi za kirafiki ambazo wamecheza wakati ligi iliposimama, zimesaidia kuwapa mazoezi mazuri wachezaji wake ambao walikutana na ushindani kutoka kwa nyota wa timu hizo zinazoshiriki ligi za madaraja ya chini.

"Mechi zimetusaidia na kutujenga pia, ndio maana tulikubali, kuna mambo tumebaini," aliongeza.

Naye Meneja wa timu hiyo, Abbas Ally, alisema wamefika salama Mbeya tangu juzi wakitokea Sumbawanga.

"Tumerudi Mbeya jana (juzi) jioni, wachezaji wote ni wazima na wamefurahia michezo ya kirafiki na utalii wa ndani wa mbuga zetu tuliofanya," alisema meneja huyo.

Simba ndio vinara wa ligi hiyo inayoshirikisha klabu 16 baada ya kuwa na pointi 19 sawa na Azam FC, wakati mabingwa watetezi Yanga ambao Jumapili wataikaribisha Mbeya City wao wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 17 sawa na Mtibwa Sugar.