Omog ataja siri mauaji Ligi Kuu

03Aug 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Omog ataja siri mauaji Ligi Kuu
  • ***Amchambua Okwi ndani nje na kubaini anapojikwaa kisha asema...

WAKATI kikosi chake kikishuka dimbani leo kucheza mechi ya pili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ametamba kwa kutaja mambo mawili yatakayowabeba katika Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Sauzi, Omog alisema kuwa muda uliobakia kabla ya kuanza kwa ligi unamtosha kuboresha wachezaji wake ambao wameripoti kwa muda tofauti kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko jijini Johannesburg.

Aidha, Omog alitaja mambo mawili yatakayowabeba Ligi Kuu kuwa ni mosi kutokana na kikosi chake kuiva na pili kuwapo kwa wachezaji wazoefu.

Alisema kabla ya kurejea nchini Jumamosi, tayari nyota wa kikosi hicho watakuwa wameelewana na kucheza mfumo ambao ameuandaa wa kuhakikisha wanashinda kila mechi watakayocheza msimu ujao.

"Tumepoteza mechi dhidi ya Orlando Pirates, kwangu ni sehemu ya kujiimarisha kiufundi, wachezaji wachache waliwahi kambini, lakini sasa nazungumzia kikosi kimekamilika, tutakuwa tofauti na tulivyocheza jana (juzi) tutakaporudi Dar es Salaam, ila kwa suala la ligi, ondoa shaka," alisema Omog alipozungumza na gazeti hili jana.

Kocha huyo aliongeza kuwa amefurahishwa na kiwango cha mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi ambaye alijiunga na kambi hiyo Ijumaa iliyopita.

"Yuko vizuri, si kama mchezaji ambaye ametoka nyumbani, amenivutia na kwake kuna vitu vichache anahitaji kuvifanyia kazi," aliongeza Mcameroon huyo.

Alisema kuwa katika mchezo wa leo atatoa nafasi kwa wachezaji ambao hawakucheza mechi iliyotangulia na hiyo ikiwa ni kulenga kufanya tathmini ya kila mchezaji.

Simba itaikaribisha Rayon Sport katika tamasha lake la Simba Day ambalo litafanyika Agosti 8, mwaka huu na kuingia kambini tena kuwavaa mahasimu wao Yanga kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakapochezwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.

Katika mechi ya juzi dhidi ya Orlando Pirates, Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji hao.

Habari Kubwa