Omog: Madini hawatoki leo

19Mar 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Omog: Madini hawatoki leo

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatarajia kushuka dimbani kuvaana na Madini FC katika mechi ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alisema jana kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na wachezaji wake wako tayari kwa 'jukumu' moja la kusaka ushindi.

Omog alisema wanahitaji kusonga mbele hivyo, leo watapambana kwa ajili ya kutafuta matokeo mazuri huku wakiwaheshimu wapinzani wao.

"Tunaingia uwanjani kwa ajili ya kusaka ushindi, hatuwadharau wapinzani wetu kwa sababu hawashiriki Ligi Kuu, kila timu iliyofika hatua hii ni bora, tutapambana dakika zote," alisema Omog.

Kocha huyo aliongeza kuwa kila mchezaji anafahamu umuhimu wa mchezo huo kwa sababu wanajua ushindi utawapeleka katika hatua inayofuata.

Katika mechi ya michuano hiyo ya Kombe la FA iliyopigwa jana, Mbao FC imekuwa ya kwanza kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuifunga Kagera Sugar kwa mabao 2-0.

Michuano hiyo itaendelea tena hapo baadaye kwa Yanga kuikaribisha Tanzania Prisons huku Azam FC ikiivaa Ndanda kutoka Mtwara.

Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo ambayo mshindi atapata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho mwakani.

Habari Kubwa