Omog: Tatizo vipigo viwili Simba hili hapa

11Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Omog: Tatizo vipigo viwili Simba hili hapa

KOCHA wa Simba, Mcameroon Joseph Omog, amesema aina ya mabao waliyofungwa kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu Bara imeonyesha safu yake ya ulinzi kukosa umakini hivyo kuna haja ya kukipangua kikosi chake.

KOCHA wa Simba, Mcameroon Joseph Omog.

Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Prisons juzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Omog, alisema safu yake ya ulinzi imekuwa dhaifu na amepanga kuwaweka benchi baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza.

"Lazima tufanye mabadiliko haraka..., tumefungwa mabao ya kizembe na yote yametokana na umakini mdogo wa safu yetu ya ulinzi," alisema Omog.

Alisema atayafanyia kazi makosa yote katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

"Kutakuwa na mapumziko mafupi na baada ya hapo tutaanza programu yetu kuelekea kwenye mzunguko wa pili," alisema Omog.

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Tanzania Prisons, ambao Simba walilala 2-1, mabao yote yalifungwa kwa kichwa kufuatia mipira ya krosi.

Mbali na mchezo huo, pia Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa African Lyon wiki iliyopita ambapo bao pekee la Lyon lilifungwa kutokana na mpira wa krosi.

Pamoja na kupoteza mchezo wa juzi, Simba bado inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 35 kufuatia michezo 15 waliyocheza ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 33 baada ya kuichapa Ruvu Shooting jana katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Habari Kubwa