Omog: Tutaivaa Azam kivingine

30Aug 2017
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Omog: Tutaivaa Azam kivingine

KOCHA wa Simba, Mcameroon Joseph Omog, amesema kuwa anaamini mchezo wao ujao dhidi ya Azam FC utakuwa mgumu na hivyo ameandaa mkakati maalum kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

KOCHA wa Simba, Mcameroon Joseph Omog.

Omog alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mwandishi wetu, kuhusu mbinu alizoandaa kuelekea mechi hiyo ya pili kwao Ligi Kuu Bara.

Alisema licha ya Azam kuondokewa na wachezaji wake waandamizi, bado anaamini wana timu nzuri inayoweza kuwapa upinzani mkubwa.

Omog alisema wataingia uwanjani wakiwa na tahadhari kubwa na watacheza kwa umakini ili kuhakikisha wanaendeleza kazi waliyoanza nayo msimu huu.

“Kuna mbinu au mipango ambayo naandaa ili kuhakikisha tunapata ushindi dhidi ya Azam, sitarajii kuona mchezo rahisi, utakuwa mgumu lakini ni lazima tupambane kupata ushindi,” alisema Omog.

Aidha, alifafanua kuwa hakuona sababu ya kuwapa mapumziko wachezaji wake baada ya baadhi ya wachezaji wake kuitwa kwenye timu ya taifa.

“Nilitaka tuendelea na mazoezi kwa sababu hata wale waliopo kwenye timu ya taifa wanafanya mazoezi kwenye kambi yao, nataka kuona hali ya hamasa inaendelea kwa wachezaji wangu,” aliongeza kusema Omog.

Simba inajipanga kuhakikisha inapata ushindi wao wa pili mfululizo tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Jumamosi iliyopita. Katika mchezo wao wa kwanza waliibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.