Omog yupo sana Mtibwa Sugar

02Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Omog yupo sana Mtibwa Sugar

LICHA ya matokeo mabaya inayopata Mtibwa Sugar kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, ataendelea kukinoa kikosi hicho, kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thobias Kifaru.

Mtibwa juzi ilifungwa bao 1-0 na Azam FC kwenye mchezo wake wa saba wa Ligi Kuu msimu huu, na inaendelea kuburuza mkia ikiwa na pointi mbili baada ya kupoteza mechi tano na kutoka sare mbili.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kifaru alisema wapo kwenye wakati mgumu, lakini bado wana imani na kocha wao, Omog kuendelea kuliongoza Jahazi hilo.

“Tuna mkataba na Joseph Omog wa miaka miwili, hivyo tutaendelea kuwa naye, tunaamini huu ni upepo mbaya tu na utapita na hali itakuwa sawa tu,” alisema Kifaru.

Alisema wanaamini uwezo wa Omog ambaye aliwahi kuzinoa Simba na Azam FC kwa nyakati tofauti.

“Omog ni kocha mkubwa na mwenye rekodi za aina yake. Kumbuka yeye ndiye alikuwa kocha mzawa pekee wakati anaiongoza nchi yake Cameroon kwenye michuano ya Afcon iliyopita hivyo tuna imani naye,” alisema.

Wakati huo huo, Kifaru amesema kuwa kwa sasa uwanja wao umefikia asilimia 80 ya maboresho na hivyo anaamini pengine mchezo wao unaofuata wa Ligi Kuu wanaweza kucheza katika uwanja wao wa nyumbani kama ukifunguliwa.
Uwanja huo ulifungiwa na bodi ya ligi nchini (TPLB) ili kufanyiwa maboresho zaidi.

Habari Kubwa