Orlando yamnyemelea usajili wa Onyango Simba

20Apr 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Orlando yamnyemelea usajili wa Onyango Simba

KLABU ya Orlando Pirates ya Ligi Kuu Afrika Kusini, imetajwa kumtaka beki kisiki wa Simba, Mkenya Joash Onyango, kutokana na kuvutiwa na kiwango chake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara, amesema alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni kiongozi wa klabu hiyo na kumuulizia kama wanaweza kumsajili.

"Niwaibie siri, jana (juzi) Meneja wa Orlando Pirates alinipigia simu na kuniambia wamevutiwa na Onyango. Kaniuliza wakimtaka mchezaji huyo ofa yake bei gani na mimi nikawatania labda walete dola milioni moja," alisema Manara.

Manara alisema kwa sasa hawezi kutaja kiasi halisi cha gharama ya Onyango, lakini hawezi kuuzwa kwa pesa ndogo kwa sababu ni mmoja wa mabeki ghali na bora Afrika kwa sasa.

"Hivi majuzi tu kachaguliwa kuwa mmoja wa mabeki bora Afrika unafikiri atauzwa bei gani?" Alisema.

Katika hatua nyingine, Manara alisema kuwa kwa sasa Simba imekuwa ikifuatiliwa si Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati tu, bali Afrika nzima na wachezaji wake pia wamekuwa wakifuatiliwa kwa karibu na klabu zote Afrika.

"Kuna mtaalam mmoja nchini Kenya ameandika kuwa Simba inaweza kuwa ni alama ya klabu zote za Ukanda wa Afrika Mashariki na ni kweli kwa sababu uwekezaji umefanyika. Myonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, bila Mohamed 'Mo' [Dewji], sisi wanachama na mashabiki wa Simba tungeweza kumlipa mchezaji Luis Miquissone? Tunaweza kumlipa Chama?" Alihoji.

Amebainisha kuwa wachezaji wa Simba, benchi la ufundi na wafanyakazi wote wa klabu ya Simba mishahara yao kwa pamoja inazidi kiasi cha Sh. milioni 300 kwa mwezi.

"Mo amekuwa akilipa mishahara ya wafanyakazi wote wa Simba, kuanzia wachezaji, benchi la ufundi hadi sisi,  Sh. milioni 300 kila mwezi, ni kama wizara tu. Ndiyo maana ninawaambia Simba kwa sasa ni dude kubwa. Halafu kuna mtu anakuja anamsema vibaya Mo. Nadhani hajui nini anachokisema," alisema Mkuu huyo wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba.

Habari Kubwa