Pablo atoa siri ushindi Kagera Sugar

13May 2022
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Pablo atoa siri ushindi Kagera Sugar

KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco, amefichua siri ya ushindi wao dhidi ya Kagera Sugar kuwa ni kuingia na mbinu tofauti hali ambayo iliwafanya wamepata ushindi wa mapema.

KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco.

Wakati Pablo akisema hayo Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Francis Baraza amesema Simba iliwazidi ujanja kwa kuziba njia ambazo wangeweza kupata ushindi.

Simba ilifanikiwa kulipa kisasi dhidi yaa Kagera Sugar kwa kuifunga mabao 2-0 katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania uliopigwa juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Pablo alisema hakuwa na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kubadili mbinu kwa wachezaji wake dhidi ya Kagera na kufunga mabao ya mapema.

“Kipindi cha kwanza tulipata ushindi wa mapema hilo lilikuwa jambo la kwanza na kipindi cha pili niliwaambia kwamba wanapaswa wapate muda wa kupumzika na kucheza kwa umakini,” alisema Pablo.

Aliongeza: “Ilikuwa ni ngumu  ukizingatia hakukuwa na viungo wa asili kwenye eneo la ukabaji pamoja na wale wa kutengeneza nafasi, ilibidi nije kwa mtindo wa kipekee na tulishinda mchezo wetu,” alisema Pablo.

Alisema amelazimika kubadili mbinu hizo kwa sababu ya asilimia kubwa ya viungo wake kuwa majeruhi na wengine kupewa mapumziko mafupi kutokana na kutoka katika matibabu.

Kikosi cha Simba kimerejea kambini jana kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa hatua ya robo fainali ya kombe la Shirikisho dhidi ya Pamba FC, utakaopigwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Naye Kocha wa Kagera, Baraza aliwapongeza vijana wake licha ya kukubali kichapo hicho.

 “Ukiangalia kipindi cha kwanza tulifanya makosa na Simba wakatumia kufunga mabao ya mapema lakini wamekuwa wajanja sana kwa sababu kipindi cha pili tulicheza vizuri na Simba wamekuwa wajanja na kugoma kuingia katika mtego wetu,” alisema Baraza.

Habari Kubwa