Pemba kuinua utalii akimuunga mkono JPM

16Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
PEMBA
Nipashe
Pemba kuinua utalii akimuunga mkono JPM

KUFUATIA juhudi mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, promota wa michezo na mitindo Mtanzania anayeishi Uganda, Jackson Pemba, amesema anatarajia kurejea nchini kuwekeza katika sekta ya utalii.

Pemba aliliambia gazeti hili kuwa, Rais Magufuli ameimarisha amani na umoja wa kitaifa, hivyo anajiandaa kuleta wawekezaji kwenye sekta ya utalii na atasaidia kuwashawishi wawekezaji wengine kuwekeza katika biashara ya hoteli, ambayo itasaidia kuinua pato la nchi.

"Niko karibu sana na mmiliki wa hoteli maarufu duniani za Marriots, tayari nina mialiko ya serikali za nchi za Malawi na Botswana, ili nao waangalie fursa na uwekezaji wa nchi hizo nilizozitaja awali," alisema Pemba.

Aliongeza anapenda kuona kazi zake zinafanyika kwa kiwango cha juu, zilizofanyiwa utafiti kila wakati na kukuza dhana za biashara, ambazo zingevutia masoko yake lengwa kufungua njia mpya na pia kurudisha kwa jamii.

Alisema, katika mipango yake ya kukuza michezo nchini, ameanzisha kampuni iitwayo Pemba Sports Africa na tayari imeshafanya kazi mbalimbali Uganda.

"Mimi ni wakala wa michezo mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15, hamu yangu ni kuendeleza urithi wa michezo wa baba yangu (Cuthbert Pemba), ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Simba ya Dar es Salaam, Tanzania,” alisema Pemba ambaye aliwahi kufanya majaribio kwenye akademi ya Carlyle United na New Castle United zote za England.

Alieleza anatarajia pia, kutumia urafiki wake na wachezaji wakongwe wa England, kama Alan Shearer, Luis Ferdinand, Kevin Keegan, Warren Burton, Robert Lee, John Barnes na Stuart John Hall, ili kukuza michezo ya ndani.

Mbali na kuweka nguvu kwenye soka, pia anamiliki timu ya mpira wa kikapu ya Pemba Warriors, huku kituo chake kikishiriki katika mashindano ya magari ya Omutima na vile vile anasimamia timu ya soka ya taasisi ya Selimundu.

"Lengo letu ni kubadilisha na kuwezesha tasnia ya michezo nchini Tanzania, kwa kutoa huduma muhimu za kimkakati kwa klabu za michezo kitaalamu, mashirikisho ya kitaifa, watu binafsi na kampuni zinazovutiwa na michezo," alisema Pemba.

Mfanyabiashara huyo pia ni rais wa WFM, kampuni ya kimataifa ambayo huwatafutia mapambano ya kimataifa mabondia wa kickboxing duniani.

Habari Kubwa