Penalti ya Kagere yaua shabiki Dar

27Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Penalti ya Kagere yaua shabiki Dar

PENALTI aliyokosa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere wakati Simba ikiitoa Stand United kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 3-2 kwenye mechi ya hatua ya 16-Bora, ya Kombe la FA, imesababisha kifo cha shabiki wa timu hiyo, mkazi wa Jeti- Lumo jijini Dar es Salaam, Pacience Mhagama.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga juzi, timu hizo zilizoka sare ya bao 1-1 baada ya dakika 90, ndipo changamoto ya mikwaju ya penalti ilipochukua nafasi yake na Kagere akiwa mpigaji wa tuta la kwanza, alikosa.

Hata hivyo, Claotus Chama, Deo Kanda na Hassan Dilunga walifunga penalti zao huku Ibrahim Ajibu naye akikosa, lakini Stand United nayo ikajikuta ikikosa tatu na hivyo Simba kutinga hatua ya robo fainali.

Akizungumza na mwandishi wetu, mtoto wa marehemu Mhagama, Edwin alisema baba yake alikuwa akiangalia mechi na rafiki zake nyumbani na baada ya Kagere kukosa penalti alianguka ghafla na kupoteza fahamu.

"Mimi sikuwa nyumbani, ila marafiki zake waliokuwa wakiangalia naye mechi hiyo walinipigia simu na kunieleza kuwa baba ameanguka ghafla baada ya Kagere kukosa penalti na amepoteza fahamu.

"Wakati wanamkimbiza hospitali alifariki dunia wakiwa njiani, hivyo kwa sasa maiti ipo Hospitali ya Temeke na tunafanya taratibu ya kusafirisha kwenda kuzika Songea (kesho) leo," alisema Edwin.

Hata hivyo, alisema enzi za uhai wake baba yao aliyefariki akiwa na umri wa miaka 62, alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo.

Habari Kubwa