Penalti ya kwanza Ligi Kuu Bara 'yaota mbawa'

16Oct 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Penalti ya kwanza Ligi Kuu Bara 'yaota mbawa'

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa katika raundi ya sita, penalti ya kwanza iliyotolewa kwenye mechi kati ya KMC FC dhidi ya Coastal Union ya jijini Tanga 'imeota mbawa'.

Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Coastal Union ilibahatika kupata penalti dakika ya 43, baada ya beki mmoja wa KMC kuushika mpira katika harakati za kuokoa, ikiwa ni penalti ya kwanza kupatikana msimu huu.

Hata hivyo, penalti hiyo iliyopigwa na Yusuph Soka iliokolewa kwa ustadi na kipa wa KMC, Juma Kaseja ambaye kwa miaka mingi anasifika kwa kuokoa mipira ya aina hiyo.

Katika mechi hiyo, KMC na Coastal Union zilitoka sare, bila kufungana kwenye moja ya mechi za ligi.

Msimu uliopita penalti ya kwanza ilipatikana kwenye raundi ya nne na mabingwa watetezi, Simba ndiyo iliyobahatika kuipata kwenye mechi kati ya timu hiyo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Septemba 26, mwaka jana.

Tofauti na penalti ya kwanza msimu huu kuokolewa na kipa, lakini hiyo ilitinga nyavuni, ikifungwa na straika wake hatari, Meddie Kagere dakika ya 78 ya mchezo, Simba ikishinda mchezo huo kwa mabao 3-0.

Azam FC yenye pointi 13 ndio inayoongoza katika msimamo wa ligi hiyo yenye kushirikisha timu 18 ikifuatiwa na Simba, Yanga, Biashara United ya Musoma na KMC wakati JKT Tanzania, Ihefu na Mbeya City zinaburuza mkia.

Ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itaendelea tena leo kwa Dodoma Jiji FC kuwakaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Jamhuri.

 

 

Habari Kubwa