Penalti ya Yanga kuna tatizo - Refa

27Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Penalti ya Yanga kuna tatizo - Refa

WAKATI Kocha wa KMC FC, Habibu Kondo, akieleza penalti tata iliyotolewa na Mwamuzi Ramadhani Kayoko wa Dar es Salaam katika mchezo wao dhidi ya Yanga, ndiyo ilichangia kuwaondoa mchezoni wachezaji wake na kujikuta wakipoteza kwa mabao 2-1 juzi, Refa mstaafu, Omar Abdulkadir, amesema "kuna tatizo".

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza juzi, Yanga ilishtukizwa kwa kufungwa bao dakika ya 26 kupitia kwa Hassan Kabunda kwa shuti kali nje ya 18, kabla ya Tuisila Kisinda kuisawazishia timu yake kwa mkwaju wa penalti dakika ya 41 akimtesa kipa mkongwe Juma Kaseja baada ya refa Kayoko kudai straika Mghana Michael Sarpong aliangushwa ndani ya boksi.

Dakika ya 61, WaziriI Junior akaifungia Yanga bao la pili likiwa ni la kwanza kwake msimu huu tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea Mbao FC, hivyo kuifanya KMC kutoka kichwa chini.

Lakini kocha Kondo, akizungumzia ushindi huo wa Yanga, alisema tatizo ilikuwa ni penalti hiyo ambayo kwake anaona haikuwa halali na kwamba ndiyo iliyowarudisha wapinzani wao mchezoni na hatimaye kushinda.

"Tatizo kwetu lilikuwa ni bao la pili, tumefanya makosa tukafungwa, ila la kwanza haikuwa penalti, kawapa wakafunga ikawarudisha mchezoni, lakini hamna shida ligi ni kama marathon bado mechi nyingi kwetu zimebaki 30," alisema. 

Lakini refa mstaafu, Abdulkadir, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Saa 72 ya TFF, alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu penalti hiyo, alisema kuna tatizo la waamuzi Tanzania, ila hawezi kuizungumzia kabla hawajakaa katika kamati hiyo.

"Nimeangalia sana, ila Tanzania kuna tatizo kubwa, hakuna waamuzi, siwezi kuizungumzia kwa sasa, kabla ya kamati kukaa, nikiongea lolote kwa sasa itakuwa si sahihi," alisema Abdulkadir huku akifafanua kuwa kamati hiyo hukutana kila wiki.

Habari Kubwa