Pesa za Samatta, Okwi zijenge uwanja Simba

08Feb 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Pesa za Samatta, Okwi zijenge uwanja Simba

KLABU ya Simba inatarajiwa kupata malipo ya wachezaji wake wa zamani, Mbwana Samatta na Emmanuel Okwi zaidi ya Sh. Milioni 900.

Sh. milioni 372 zinatokana na mauzo ya Samatta kwenye klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji kutoka TP Mazembe ya Congo DR. Pesa hizo ni asilimia 20 ya mauzo ya mchezaji huyo, ambayo Simba inatakiwa ipate kutokana na makubaliano ya mkataba wa klabu hiyo ilipowauzia mwaka 2011.Chini ya uongozi wa Ismail Aden Rage, Simba ilimuuza Samatta, mbali na pesa za mauzo, lakini kulikuwa na kipengele cha kupata asilimia 20 atakapouzwa kwenye klabu nyingine.Miaka miwili baadaye, 2013 chini ya uongozi wa huyo huyo Rage Simba ilifanya biashara nyingine ya kumuuza Okwi kwenye klabu ya Etoile du Sahel. Hata hivyo, klabu hiyo haikufanya uungwana na wamechukua muda mrefu kiasi cha Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuingilia kati na kuamuru Etoile kuilipa Simba ndani ya siku 60, vinginevyo adhabu mbalimbali zitawashukia. Kwa maana hiyo, iwapo Simba itakusanya fedha zote hizo, itakuwa na kiasi cha pesa ambacho hakipungui Sh. milioni 900 hivi. Wanachama na mashabiki wa klabu hiyo hawategemei neema hii ikageuka balaa au mkosi kwa klabu hiyo kwa viongozi wa sasa kuanza kugombana na kusababisha mtafaruku au mgogoro usio wa lazima. Hawatowaelewa viongozi kuwa pesa hizo badala ya kuifanya klabu yao kuinuka angalau kidogo kiuchumi. Tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, imeshindwa kuwa na uwanja angalau wa kufanyia mazoezi, achilia mbali wa mechi. Ushauri wangu kwa viongozi wa Simba ni kuwa zitakapotua pesa hizo, kitu cha maana ambacho kitawajengea heshima kwa kutengeneza eneo lao la Bunju ili uwe uwanja wa kufanyia mazoezi. Mwishoni mwa mwaka jana klabu hiyo ilitangaza kuwa ingeanza kufanya kazi hiyo kuanzia Januari kwa pesa za mfadhili mmoja, lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote ile. Kwa kuwa pesa za klabu zinatarajia kuwasili, nadhani hilo ndilo litakuwa suluhisho. Pesa hizo zinaweza kabisa kuuliendeleza eneo kwa kuchimba kisima cha maji ambacho kitakuwa kinahudumia uwanja huo, kujenga uzio ambao utawafanya wanachama na mashabiki wa timu hiyo kutoa angalau kiingilio kidogo kwa ajili ya kuichangia timu yao wanapokwenda kutazama mazoezi. Pia pesa hizo zinaweza kutumika kuweka vizuri miundombinu ya uwanja huo kuwa mizuri na kuvutia watu wengine kutaka kufanya biashara kama ya vinywaji, chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu. Nina uhakika kuwa kama viongozi wa Simba wakifanya hivyo, si tu kwamba majina yao yatabaki kuwa kumbukumbu ya vizazi na vizazi kwenye historia ya klabu hiyo, lakini pia itawafanya kutengeneza kitega uchumi ambacho kinaweza kabisa kuyarudisha mamilioni hayo watakayotumia. Kwanza kabisa wataifanya klabu hiyo kuwa na uwanja wake wenyewe wa mazoezi, hivyo kuendana na matakwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linalotaka kila klabu kuwa leseni na ili kuipata moja ya vigezo ni lazima kuwa na uwanja wa mazoezi. Pia wanachama na mashabiki wa klabu hiyo hawatolazimika kuanza kuuliza timu yao inafanya mazoezi wapi, bali watakuwa wakimiminika kwenye uwanja huo na kutoa kiingilio ambacho kikikusanywa kinaweza kuhudumia wachezaji hata kuwanunulia maji na mahitaji mengine madogo madogo. Viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wakitumia pesa nyingi kwa ajili ya kukodi viwanja vya kufanyia mazoezi. Najua kuwa klabu ya Simba ina madeni, lakini pesa za wachezaji hao zisitumike kulipia madeni hayo na badala yake zifanyiwe kitu ambacho kitabaki kuwa historia. Kama ni madeni basi yalipwe kutokana na viingilio vya uwanjani na si pesa za Samatta na Okwi ambazo Wanasimba wote watataka kuona zinatumika vipi, na matumizi yake wayafanye watembee kifua mbele. Huu ni ushauri wangu kwa viongozi wa klabu hiyo kongwe kama kweli wanaguswa na umaskini wa kutokuwa na uwanja wa mazoezi. Yeyote anayetaka kufungua shule ni lazima kwanza awe na majengo, iweje klabu kubwa ya mpira wa miguu kama Simba isiwe na uwanja wake walau wa mazoezi?

Habari Kubwa