Phiri ajitetea kipigo cha City Tanga

16Mar 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Phiri ajitetea kipigo cha City Tanga
  • Timu hiyo ya Mbeya juzi ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya African Sports, kikiwa ni kipigo cha 11 Ligi Kuu msimu huu.

BAADA ya kushuhudia Mbeya City FC ikilala 2-0 dhidi ya African Sports juzi, kocha mkuu wa timu hiyo ya Mbeya, Kinnah Phiri, amejitetea kuwa hali ya hewa ilikuwa kikwazo kwa timu yake.

kocha mkuu wa timu hiyo ya Mbeya, Kinnah Phiri.

Mabao mawili yaliyofungwa ndani ya dakika saba kipindi cha pili na mshambuliaji Omary Issa yaliandikisha kipigo cha 11 kwa City Ligi Kuu msimu huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuitoa Sports mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa nafasi moja.

Akizungumzia mechi hiyo jana, Phiri alidai kuwa hali nzito ya hewa jijini Tanga ilikuwa changamoto kubwa kwa timu yake inayoshika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.

"Hatukuwa na hali nzuri kimchezo, hewa ilikuwa na ilituathiri sana," alisema. "Tulicheza tukiwa kwenye joto kali, lakini hayo ndivyo matokeo ya soka. Tulichokitarajia hakikuwa.

"Tunakwenda Songea kucheza mechi nyingine ngumu, imani yangu tunaweza kupata ushindi huko."

Kipigo cha juzi kilikuwa cha nne (tatu Ligi Kuu) kwa kocha huyo mpya wa City tangu ajiunge na klabu hiyo mwezi uliopita akishinda 5-1 dhidi ya Toto Africans, 2-0 dhidi ya Stand United na vipigo dhidi ya Azam FC (3-0), Simba (2-0) na Prisons (2-1 Kombe la FA).

Habari Kubwa