Pluijm aanza tambo Singida Utd

14Sep 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Pluijm aanza tambo Singida Utd

BAADA ya kushuhudia timu yake ikiibuka na ushindi wa kwanza Ligi Kuu wiki iliyopita, kocha wa Singida United inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri matokeo ya SportPesa, Mholanzi Hans van der Pluijm, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kudai sasa 'chama' lake limeanza kazi.

Hans van der Pluijm.

Singida ilianza Ligi Kuu kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mwadui FC kabla ya wiki iliyopita kupata ushindi kama huo dhidi ya Mbao FC katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Pluijm, aliliambia Nipashe kuwa walianza vibaya Ligi Kuu iliyoanza Agosti 26, mwaka huu kutokana na kuwa na majeruhi kwenye kikosi chake.

"Baadhi ya wachezaji wangu hawakuwa kwenye viwango vyao, na hii ilitokana na kuumia, lakini kwa sasa mambo yanakaa sawa," alisema Pluijm.

Alisema ushindi wa mchezo uliopita ni ishara kuwa kwa sasa timu yake inakaa kwenye mstari na itaendelea kupambana kuhakikisha inafanya vizuri.

"Ukimuondoa golikipa Ally Mustapha (Barthez), wachezaji wengine wote wapo kwenye hali nzuri, wengi wamepona na baada ya mazoezi ya siku hizi zilizobaki nitaona nani atacheza kwenye mchezo wetu wa Jumamosi ijayo," alisema Pluijm.

Singida United inayotumia Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma kama Uwanja wake wa nyumbani, ilitegemea kuondoka jana Dodoma kuelekea Shinyanga tayari kwa mchezo wao dhidi ya wenyeji wao Stand United utakaochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage.

Habari Kubwa