Pluijm sasa aipania Simba

12Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Pluijm sasa aipania Simba

BAADA ya kutupwa nje kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, Kocha wa Singida United, Mholanzi Hans van der Pluijm, amesema kazi inayofuata sasa ni kujiandaa kuivaa Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha wa Singida United, Mholanzi Hans van der Pluijm.

Singida United ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Azam FC, katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa Uwanja wa Amaan juzi usiku, hivyo kuungana na Yanga na Simba ambazo nazo zimeyaaga mashindano hayo.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kasi na kushambuliana kwa zamu kwa kipindi chote cha dakika 90, Azam ililazimika kusubiri hadi dakika ya 78 kupata bao hilo pekee kupitia kwa mtokea benchi Braison Raphael.

Akizungumza na Nipashe mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Pluijm licha ya kuipongeza Azam FC kwa ushindi huo, aliwapongeza pia wachezaji wake kwa kuonyesha kandanda safi na kueleza amepata fursa ya kuwajaribu wachezaji waliokuwa hawapati nafasi.

“Nimepoteza mechi yangu ya kwanza katika michuano hii, na ninawapongeza wachezaji wangu kwa kuonyesha uwezo na kufuata maagizo yangu.

“Kikubwa ni kwamba michuano hii imetusaidia kujua uwezo wa wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi mara kwa mara,” alisema Mholanzi huyo na kuongeza.

“Sasa tunakwenda kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, na michuano hii imetupa fursa ya kutambua wapi tunapaswa kupafanyia kazi.”

Pluijm alisema anafahamu mechi dhidi ya Simba haitakuwa rahisi, hivyo moja kwa moja wanaenda kufanya maandalizi ili kuhakikisha wanapata matokeo katika mchezo huo.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kama ilivyo kwa Singida United na Yanga, itakialika kikosi hicho cha Pluijm kwenye Uwanja wa Uhuru Alhamisi ya Januari 18, mwaka huu.

Habari Kubwa