Pochettino azungumzia tetesi kutua Man United

25Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Pochettino azungumzia tetesi kutua Man United

MAURICIO Pochettino amesema majaliwa yake "hayana shaka" kwani ana furaha pale Paris Saint-Germain huku ripoti zikimhusisha na Manchester United kwenda kuchukua nafasi ya Ole Gunnar Solskjaer.

United walimfukuza Solskjaer Jumapili baada ya kufungwa mabao 4-1 na Watford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England na Michael Carrick amechukua nafasi ya kuisimamia timu hiyo kwa muda.

'Mashetani Wekundu' hao waliripotiwa kupanga kuteua kocha wa muda hadi mwishoni mwa msimu huu, lakini uvumi umeongezeka kwamba wanafanya mazungumzo na Pochettino ili kupewa mikoba hiyo.

Kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Pochettino alisisitiza haangalii uwezekano wa kuondoka PSG.

Aliwaambia waandishi wa habari Jumanne: "Nafikiri ilikuwa wazi kabisa. Nilisema kwamba, nina mkataba hadi mwaka 2023. Msimu huu na msimu unaokuja.

“Nina furaha hapa PSG. Ni ukweli. Hakuna mashaka yoyote, nina furaha hapa Paris."

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 49 raia wa Argentina, ambaye alichukua mikoba ya kuinoa PSG Januari, ameongeza kusema kwamba, kwa sasa akili yake ni katika kazi aliyonayo.

Alipoulizwa kuhusu kuhusishwa na Man United, alisema: "Hatupo hapa kuzungumzia kuhusu hilo. Naiheshimu klabu yangu PSG. Kitu kingine kinachofanywa na klabu nyingine mimi hakinihusu.”

"Sitazungumza lolote kuhusu hilo, kwa sababu hata nisipozungumza nitaandikwa tu.”

Habari Kubwa