Polisi Tanzania, KMC vitani kwa Matola

11Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi Tanzania, KMC vitani kwa Matola

BAADA ya timu yao kupanda daraja la kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Polisi Tanzania umeacha mchakato wa kuboresha benchi lake la ufundi na limeanza kwa kumwania Kocha wa Lipuli FC, Selemani Matola, imefahamika.

Kocha wa Lipuli FC, Selemani Matola.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinaeleza kuwa tayari uongozi wa Maafande hao wa Jeshi la Polisi wameshafanya mazungumzo ya awali na Matola na sasa wanasubiri majibu kutoka kwa kiungo huyo wa zamani wa Simba.

Chanzo chetu kiliendelea kueleza kuwa Matola aliwataka viongozi wa Polisi Tanzania wasiwe na wasiwasi kutokana na maombi yao na kuwaambia atawapa jibu baada ya kupitia ofa wanazotarajia kumpa endapo atakubali kusaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo.

"Ni kweli nimefuatwa na KMC, na sasa Polisi Tanzania, lakini bado sijafanya uamuzi kuhusu wapi nitafanya nao kazi," alisema kwa kifupi Matola.

Kocha huyo aliongeza kuwa pia anaendelea na mazungumzo dhidi ya mabosi wake wa Lipuli FC, ili asaini mkataba mpya wa kuendelea kuifundisha klabu hiyo ya Iringa.

"Hata Lipuli pia tunaendelea kuwasiliana na kuna baadhi ya majukumu bado yanafanyiwa kazi kwa kufuata mapendekezo yangu," Matola alisema.

Naye Ofisa Habari wa Lipuli, Clement Sanga, amesema kuwa baada ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita kumalizika pamoja na mechi ya fainali ya Kombe la FA, walimpa mapumziko kocha huyo pamoja na wachezaji, hivyo watatoa msimamo kuhusu hatima yake, likizo itakapomalizika.

Mbali na kucheza fainali ya FA kwa mara ya kwanza, Matola aliisaidia Lipuli kumaliza ligi ikiwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo.

Habari Kubwa