Polisi Tanzania wamtangaza Matola

15Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Polisi Tanzania wamtangaza Matola

UONGOZI wa "Maafande" wa Polisi Tanzania itakayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao imemtangaza Selemani Matola, kutoka Lipuli FC kuwa kocha wake mpya.

Selemani Matola.

Mbali na Polisi Tanzania, timu nyingine iliyopanda daraja ni pamoja na Namungo FC ya mkoani Lindi.

Matola alikuwa pia anahusishwa na mipango ya kujiunga na KMC FC ya jijini Dar es Salaam baada ya aliyekuwa kocha wake, Etienne Ndayiragije, kuhamia Azam FC.

Akizungumza jana jijini, Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi, alisema jana kuwa Matola amesaini mkataba wa mwaka mmoja na uamuzi wa kumwajiri kocha huyo umetokana na kufahamu uwezo na uzoefu wake.

Munisi alisema kuwa wanaamini chini ya Matola, kikosi chao kitaimarika na kitakuwa moja ya timu zitakazotoa ushindani katika kila mechi watakayocheza.

"Tunapenda kumtangaza rasmi, Selemani Matola, ameingia katika familia ya Polisi Tanzania, tutaahidi kumpa ushirikiano ili aweze kufanya vema majukumu yake," alisema Munisi.

Aliongeza kuwa timu hiyo ambayo ilikuwa inatumia Uwanja wa Chuo cha Polisi Moshi ilipokuwa Ligi Daraja la Kwanza, sasa itahamia mkoani Dodoma.

Matola aliliambia Nipashe kuwa anashukuru kupata nafasi ya kujiunga na Polisi Tanzania, na kwa pamoja amejiandaa kuifanya timu hiyo iwe imara na iweze kupambana katika mashindano yote watakayoshiriki.

"Nashukuru kwa kupata heshima hii, nimekubali kujiunga na timu hii na ninaamini watapata kile wanachokitarajia, kazi ya mpira inaonekana hadharani," Matola, kiungo wa zamani wa Simba Supersport ya Afrika Kusini alisema.

Msimu uliomalizika, Matola alimaliza katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kucheza fainali ya Kombe la FA.

Habari Kubwa