Presha mtanange Simba na Yanga 

25Sep 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Presha mtanange Simba na Yanga 
  • ***Zakimbiana Dar, mashabiki marufuku mazoezini, Bocco aomba radhi na kusema...

PRESHA inazidi kupanda kuelekea mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga itakayopigwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, baada timu hizo kufunga kwa wiki iliyopita kwa ushindi.

Baada ya juzi kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida United, Kocha Mwinyi Zahera, ameliambia Nipashe kuwa anataka kuiweka timu nje ya Dar es Salaam kwa kipindi kilichobakia kabla ya kukabiliana na Simba.

“Hayo ndiyo mapendekezo yangu lakini tutaangalia uongozi watasema nini,” alisema Zahera.

Alisema kuwa yapo mapungufu madogo aliyoyaona kwenye kikosi chake na kwa kutambua ukubwa wa mchezo dhidi ya Simba na upinzani uliopo, anataka kukaa na timu yake sehemu tulivu kufanyia kazi mapungufu yote.

Kwa upande wa kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kilirejea Dar es Salaam jana usiku na leo asubuhi kitaanza rasmi mazoezi kwa ajili ya mechi dhidi ya watani zao, Yanga.

Timu hiyo iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Mbelgiji, Patrick Aussems, iliondoka Shinyanga jana mchana kuelekea Mwanza kwa ajili ya kupanda usafiri wa ndege na kurejea Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally, alisema benchi la ufundi limeamua maandalizi ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi itakuwa jijini na si mahali kwingine kama ilivyozoeleka.

Ally alisema, lakini mazoezi yao yatafanyika katika uwanja ambao hautaruhusu mashabiki, lengo likiwa ni kuongeza utulivu.

"Muda huu (saa 9 : 20 mchana jana) ndio tuko njiani tunaelekea Mwanza, tutaondoka na ndege ya usiku, mwalimu amependekeza kambi iwe hapo hapo Dar es Salaam, labda ufanyike uamuzi mwingine tofauti baada ya kufika huko," alisema mratibu huyo.

Aliongeza kuwa wachezaji wote wa timu hiyo ni wazima na hakuna mchezaji mwenye adhabu ya kadi, ukiondoa nahodha na mashambuliaji wao, John Bocco ambaye alipata kadi nyekundu juzi.

"Tunamshukuru Mungu tulimaliza mchezo salama, kwa maana hakuna mchezaji aliyeumia, tuna kikosi kipana na hatuna presha yoyote kuhusiana na mechi yetu ya Jumapili," aliongeza.

BOCCO AOMBA RADHI

Nahodha huyo amewaomba radhi mashabiki na wanachama wa timu hiyo kutokana na kadi nyekundu aliyoipata ambayo itamfanya aukose mchezo wa Jumapili dhidi ya Yanga.

"Namshukuru Mungu tumemaliza mechi salama, tumepata pointi tatu muhimu, lakini napenda kuwaomba radhi mashabiki, viongozi na wachezaji wenzangu kwa tukio lililotokea jana, haikuwa dhamira yangu," alisema mshambuliaji na nahodha huyo wa zamani wa Azam FC, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu juzi baada ya kumgonga kwa ngumi mchezaji wa Mwadui wakati timu hizo mbili zilipokutana juzi na Simba kushinda mabao 3-1.

Habari Kubwa