'Prisons hakuna kukata tamaa hadi kieleweke'

18May 2022
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
'Prisons hakuna kukata tamaa hadi kieleweke'

KIPIGO cha bao 1-0 ilichokipata Tanzania Prisons juzi nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya Kagera Sugar, kimezidi kuiweka timu hiyo kwenye hali mbaya, huku Kocha Msaidizi, Shaaban Mtupa akidai bado hawajakata tamaa.

Wachezaji wa Kagera Sugar, wakimpongeza, David Luhende baada ya kuifungia bao pekee dhidi ya Tanzania Prisons dakika ya 88, kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya juzi. MPIGAPICHA WETU

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mtupa, straika wa zamani wa timu hiyo, alikiri kupoteza mechi hiyo kumewaweka kwenye wakati mgumu, lakini wanafarijika kuona hakuna yeyote mwenye uhakika wa kubaki kwa timu 14, ukiondoa timu za Simba na Yanga tu.

"Tumefungwa, ni kweli hali yetu ni mbaya, lakini hii haitufanyi kukata tamaa, tutapambana, tumebakisha mechi sita, lolote linaweza kutokea, hakuna timu yenye uhakika wa kubali Ligi Kuu kwa timu 14, kwa hiyo sisi kwa mechi zilizobaki tutafanya vema, tutabaki," alisema.

Lilikuwa ni bao lililowekwa wavuni na mtaalam wa kupiga mipira ya faulo, David Luhende, akifanya hivyo dakika tatu kabla ya mechi kumalizika.

Prisons iliyopanda Ligi Kuu mwaka 1995, kabla ya kushuka mwaka 2009, ilifanikiwa tena kurejea Ligi Kuu 2011, ambapo mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Muungano mwaka 1999.

Hata hivyo, kama Prisons isipojirekebisha, inaweza kushuka kutokana na mwenendo wake usioridhisha msimu huu.

Kwa sasa inashika nafasi ya 15, ikiwa na pointi 23, ikicheza mechi 24, kushinda sita, sare tano na kupoteza michezo 13.

Habari Kubwa