Rage: Simba SC tumelipiza kisasi

29Jun 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rage: Simba SC tumelipiza kisasi

ALIYEKUWA mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema kuwa kitendo cha klabu yake kufanikiwa kumnasa, Paschal Wawa ni sawa na kulipiza kisasi kwa watani zao Yanga ambao pia walikuwa wanamwania beki huyo wa kati kutoka Ivory Coast.

ALIYEKUWA mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.

Wawa alitua Simba mapema wiki hii lakini bado hajasaini mkataba baada ya kupewa masharti ya kuonyesha kiwango cha juu katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame yanayoanza leo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili, Rage alisema kuwa amejisikia faraja sana kuona Simba imewazidi "kete" Yanga katika mbio za kumsajili Wawa ambaye aliwahi kuitumikia Azam FC misimu miwili iliyopita.

Rage aliitakia mafanikio zaidi Kamati ya Usajili ya Wekundu wa Msimbazi kuwapata nyota wote inaowahitaji ili waweze kufanikiwa zaidi katika msimu ujao.

"Hii ndio furaha yetu, kuifanya Yanga ipepesuke na iwe dhaifu, nakumbuka walinidhalilisha sana wakati wa usajili wa Mbuyu Twite, sasa nasisi tumelipiza kisasi, na bado, kama kuna mchezaji mwingine wanamtaka nawaomba viongozi wangu wamsajili," alisema Rage.

Aliongeza kuwa Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa na ushindani zaidi hivyo ni lazima kila upande unatakiwa kujiimarisha kwa lengo la kujiandaa kufanya vizuri katika msimu ujao.

"Simba pia mwakani inashiriki mashindano ya kimataifa, lazima tuwe imara kila idara kwa sababu tunataka kufika mbali," alisema katibu mkuu huyo wa zamani wa Chama cha Soka Tanzanai (FAT sasa TFF).

Kwa sasa Simba inajiandaa kushiriki mashindano ya Kombe la Kagame ikiwa imepangwa kuanza kampeni za kuwania ubingwa wa michuano hiyo kesho kwa kucheza na Dakadaha ya Somalia. 

Habari Kubwa