Rasmi Ronaldo anaondoka United

24Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rasmi Ronaldo anaondoka United

MSHAMBULIAJI wa Timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo (37), anatarajiwa kuondoka Manchester United mara moja.

Uamuzi huo unafuatia mahojiano yenye utata ambapo aliikosoa klabu hiyo na kusema "hana heshima" kwa kocha, Erik ten Hag.

Pande zote mbili zilisema kuondoka kwa Ronaldo "ni uamuzi uliokubaliwa kwa pamoja".

"Klabu inamshukuru kwa mchango wake mkubwa katika misimu miwili ndani ya Old Trafford," ilisema taarifa ya Manchester United.

Walimtakia "yeye na familia yake heri kwa siku zijazo" na wakaongeza "kila mtu katika Manchester United anabakia kulenga kuendeleza maendeleo ya timu chini ya Erik ten Hag na kufanya kazi pamoja kuleta mafanikio uwanjani".

Ronaldo yuko pamoja na Ureno kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar na anatazamiwa kuwa nahodha wao katika mchezo wao wa ufunguzi wa Kundi H utakaochezwa leo dhidi ya Ghana.

"Kufuatia mazungumzo na Manchester United tumekubaliana kwa pamoja kumaliza mkataba wetu mapema," ilisema taarifa ya fowadi huyo.

"Ninaipenda Manchester United na ninawapenda mashabiki, hilo halitabadilika kamwe. Hata hivyo, ninahisi kama wakati mwafaka kwangu kutafuta changamoto mpya.

"Naitakia timu kila mafanikio kwa kipindi kilichosalia cha msimu huu na kwa siku zijazo."

 

 

 

 

 

Habari Kubwa