RC Arusha awafunda Washiriki Lete Raha Miss Tanzania

16Oct 2016
Faustine Feliciane
Arusha
Nipashe Jumapili
RC Arusha awafunda Washiriki Lete Raha Miss Tanzania

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amewaasa washiriki wa shindano la Miss Tanzania 2016, kuweka utu mbele badala ya fedha kwenye shughuli za kijamii watakazoshiriki mara baada ya kumalizika kwa kinyang'anyiro hicho.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Akizungumza na warembo hao ofisini kwake jana, Gambo alisema suala la utu ni muhimu katika jamii na litaleta heshima kwenye tasnia ya urembo hususani katika shindano la Miss Tanzania.

"Ninyi ndiyo mabalozi wa Miss Tanzania, na kama kutakuwa na mabaya kuhusu shindano hili washiriki wenyewe ndio mnaolibomoa kwa yale mabaya mnayoyafanya au kuyasema mara baada ya shindano," alisema Gambo.

Aidha, amewataka warembo hao kutokuwa 'rahisi', na kila uhusiano watakaouanzisha na watu au taasisi mbalimbali uwe na manufaa kwa shindano zima la Miss Tanzania.

Pia, Gambo ameipongeza kamati nzima ya Miss Tanzania kwa kufanya ziara katika mkoa wake.

"Nashauri shindano lijalo la Miss Tanzania lifanyike hapa Arusha kwa sababu ni mkoa nzuri na mtapata sapoti kubwa kutoka kwa wadau mkoani hapa," alisema Gambo.

Kwa upade wake aliyewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1999, Hoyce Temu, aliwataka washiriki hao kuzingatia umuhimu na ukubwa wa taji la Miss Tanzania.

"Taji hili si la mtu yeyote mmoja mmoja, hili ni taji la taifa na lipo kwa ajili ya kutumikia jamii," alisema Hoyce.

Shindano la Lete Raha Miss Tanzania 2016, limepangwa kufanyika Oktoba 29 jijini Mwanza, Kampuni ya The Guardian Ltd ni mdhamini kupitia gazeti lake la Lete Raha.

Wadhamini wengine ni pamoja na StarTimes, PII, Morena Hotel Dodoma, Regency Park Hotel Singida, HC pamoja na Jozi Lounge Msasani.

Habari Kubwa