RC Mtwara kushiriki mashindano ya kukuna nazi

01Dec 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe
RC Mtwara kushiriki mashindano ya kukuna nazi

MKUU wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amesema ataibuka mshindi katika mashindano ya kukuna nazi yanayotarajiwa kufanyika mkoani humo kuanzia Desemba 3 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kuelekea shamra shamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru.

Amesema licha ya mshindani wake wa karibu katibu tawala wa Mkoa Abdallah Malela kujinadi kuwa ana aina zaidi ya tatu ya ukunaji nazi ni wazi atamuonyesha ubora wake katika mashindano hayo baada ya kufanya mazoezi ya kutosha.

Gaguti, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea maandalizi ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru kimkoa yatakayofanyika katika mji wa kitalii wa Mikindani

"Mwenzangu RAS Malela, amejinasibu kushinda na kunitajia aina mbali mbali ya tui atakalotoa, lakini mimi nitamshinda katika hili ingawa mchezaji bora hawezi kupatikana katika mchezo mmoja hivyo nitamkaribisha tushindane na katika riadha pamoja na michezo ya kuogelea,” alisema Gaguti

Alieleza kuwa katika kuelekea michezo hiyo mkoa wa Mtwara imeanza kushiriki shughuli mbali mbali ikiwemo mashindano ya Insha kwa shule za msingi na sekondari,na kueleza kuwa mbali na mashindano ya kukuna nazi pia watakuwa na mashindano ya ngoma za asili, kuogelea na michezo maalum kwa watu wenye mahitaji maalum

Alisema wazee wenye miaka 60 watashiriki matembezi ya pamoja kushiriki michezo ya bao mpira wa miguu na kuvuta kamba

Aliongeza kuwa kabla ya michezo hiyo kuanza wananchi watashiriki shughuli za kijamii ikwemo kufanya usafi katika hospitali za mkoa huo pamoja na masoko

Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa huo alisema amejiandaa vya kutosha kushinda katika shindano la ukunaji nazi huku akielezea aina ya tui atakalotoa

“Unajua ukikuna nazi vizuri unapaswa ukune liwe laini na tui la kwanza linaitwa tui bubu, hili linajiongelea lenyewe na tui la pili ni tui ngenga hili halijiongeleai na ili ulipate tui bubu ni lazima ukune nazi iwe laini na siyo vipande vipande hivyo mimi ni miongoni mwa washindani tutakaoenda kushinda katika eneo hilo,” alisema Malela.

Habari Kubwa