Rekodi zatawala Prisons vs Simba

27Jun 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Rekodi zatawala Prisons vs Simba

WAKATI Prisons ikitarajiwa kuipokea Simba kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya kesho Jumapili, timu hiyo inaongoza kwa kutoa sare nyingi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu hadi kufikia jana.

Prisons inayokamata nafasi ya 10, ikiwa na pointi 42 kwa mechi 31 ilizocheza, imetoa sare mara 15 mpaka sasa ikiwa ni rekodi ya juu ambayo haijafikiwa na timu yoyote msimu huu mpaka sasa.

Maafande hao watashuka dimbani kucheza dhidi ya Simba ambayo nayo ndiyo timu iliyotoa sare chache zaidi kwenye ligi hiyo mpaka sasa, ikiwa pia ndio mabingwa watetezi.

Simba ina sare tatu tu kwenye Ligi Kuu mpaka sasa ambazo ni za mabao 2-2 dhidi ya Yanga, mzunguko wa kwanza, sare ya bila kufungana kati ya timu hizo mbili (Simba na Prisons), katika mechi ya mzunguko wa kwanza,  na ile ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting.

Katika mechi 31 ambazo imecheza, Prisons imeshinda mechi tisa, sare 15 na kupoteza michezo saba.

Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza, wanafuatiwa na Yanga ambao mpaka sasa imetoa sare mara 12 na kuwa ni moja kati ya timu yenye sare nyingi msimu huu.

Yanga inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 57, imecheza michezo 31, ambapo wameshinda mechi 15, sare 12 na kupoteza mechi nne wakati Ndanda na JKT Tanzania zinakamata nafasi ya tatu, kila moja ikiwa imetoa sare mara 11.

JKT Tanzania inayokamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 47, imeshinda mechi 12, sare 11 na kupoteza mechi nane, huku Ndanda ambayo leo inacheza dhidi ya Yanga, imeshinda mechi nane, sare 11 na kupoteza mechi 12, ikiwa na pointi 35, kwenye nafasi ya 15 wa msimamo wa ligi.

Timu nne za Namungo, Mwadui, Biashara United na Mtibwa Sugar zinafuatia kwa kila moja kutoa sare mara 10.

Namungo ipo juu ya hizo, ikishika nafasi ya nne kwa pointi 55, Biashara United ikiwa kwenye nafasi ya tisa kwa pointi 43,  Mtibwa Sugar ikiwa kwenye nafasi ya 12 kwa pointi 37 na Mwadui nafasi ya 13 kwa pointi hizo hizo 37.

Habari Kubwa