Robo fainali Umoja Cup Rorya 2021 kuanza Ijumaa

14Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Robo fainali Umoja Cup Rorya 2021 kuanza Ijumaa

MICHUANO ya Umoja Cup 2021 Wilaya ya Rorya mkoani Mara, iliyoanza kutimua vumbi mapema Oktoba mwaka huu ikijumuisha jumla ya timu 20, imetinga hatua ya robo fainali baada ya kupatikana vinara nane kutoka kila kundi.

Kikosi cha timu ya Rifa FC kinachotarajiwa kuvaana na mabingwa watetezi wa Umoja Cup, Shirati Mji, kwenye mechi ya robo fainali itakayopigwa Jumatatu ijayo katika Uwanja wa wa Maji Sota, Rorya mkoani Mara. MPIGAPICHA WETU

Katika michuano hiyo ambayo huu ni mwaka wa tisa ikifanyika Uwanja wa Maji Sota, huku ikidhaminiwa na mdau maarufu wa soka wilayani humo, Peter Owino, timu zilizofanikiwa kutinga robo fainali ni Menonnite, Watumishi, Magamaga, Rifa FC, Masonga, Kirengo, Wanamaji FC pamoja na mabingwa watetezi, Shirati Mji FC.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mashindano hayo, Obong'o Maina, hatua ya robo fainali itapigwa siku nne mfululizo, ambapo itaanza Ijumaa wiki hii kwa Menonnite kuvaana na Masonga huku Jumamosi Watumishi wakiwa na kibarua pevu dhidi ya Kirengo FC.

Jumapili itakuwa zamu ya Magamaga dhidi ya Wanamaji FC huku Jumatatu pakiwa na shughuli pevu wakati Rifa FC itakapokabiliana na mabingwa watetezi, Shirati Mji mechi zote zikipigwa katika Uwanja wa Maji Sota.

Nusu fainali ya kwanza itachezwa Novemba 27, mwaka huu, kwa mshindi kati Menonnite na Masonga kukutana na timu itakayoshinda kati ya Watumishi na Kirengo FC, wakati nusu fainali ya pili ikipigwa kesho yake kwa mshindi kati ya Magamaga na Wanamaji FC kuchuana na mshindi dhidi ya Rifa FC na Shirati Mji.

Obong'o alisema mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itapigwa Desemba 3, kabla ya fainali ya michuano hiyo ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Rorya na vitongoji vyake, kupigwa Desemba 5, mwaka huu.

Akizungumzia michuano hiyo kwa ujumla hadi sasa, Obong'o alisema timu nyingi zimeonyesha kusikitika baada ya kushindwa kutinga robo fainali, huku akielezea Bubombi FC ambayo pamoja na kutoa upinzani mkubwa haikuweza kufurukuta mbele ya Shirati Mji na Kirengo FC, ambazo zote zimewahi kutwaa ubingwa huo.

Alisema licha ya timu ya Minigo FC kutoka mbali, imeshiriki kikamilifu na imeonyesha nidhamu ya hali ya juu, hii ikiwa ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo ya Umoja Cup.

"Minigo wamekiri kujifunza mengi kupitia michuano hii huku wakiweka wazi kuwa walidhani Umoja Cup ni mashindano madogo, lakini visiki walivyokutana navyo vimewanufaisha katika soka kwa kuwa wao bado vijana wadogo wanayo nafasi kwa baadaye.

Aidha, Obong'o alisema hadi sasa wachezaji wanaoongoza kwa kufumania nyavu ni Omity wa Wanamaji fc, aliyetupia mabao matano akifuatiwa na Sande Olise wa Rifa FC mwenye mabao manne.

Alisema changamoto wanayokabiliwa nayo kwa sasa ni ya ulinzi kutokana na mashabiki kuwa wengi na kila mmoja akitaka timu yake ishinde na matokeo yanapokuwa tofauti ndiyo huwa kazi kuwadhibiti.

Habari Kubwa