Ruvu Shooting kuitibulia mazoezi Simba

02Jun 2020
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Ruvu Shooting kuitibulia mazoezi Simba

BAADA ya ratiba ya Ligi Kuu inayotarajiwa kurejea Juni 13, mwaka huu kutokana na Simba kupangwa kuanza dhidi ya Ruvu Shooting, benchi la ufundi la mabingwa hao watetezi limesema litakutana kutazama namna ya kubadili programu ya mazoezi tayari kwa ajili ya kuivaa miamba hiyo ya Pwani.

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), jana ilitangaza ratiba mpya ya ligi hiyo ambayo ilisimama tangu Machi 17, mwaka huu kutokana na mlipuko wa maambukizo ya virusi vya corona, ambapo sasa inarejea Juni 13 kutokana na serikali kujiridhisha na kushuka kwa maambukizo na wagonjwa waliokuwa hospitalini kupona.

Katika ratiba hiyo iliyotangazwa jana na Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo, Simba imepangwa kuanzia Uwanja wa Taifa Juni 14, mwaka huu dhidi ya Ruvu Shooting wakati Azam FC yenyewe ikiikaribisha Mbao FC kwenye dimba lao la Azam Complex, ikiwa ni siku moja baada ya Yanga kushuka katika dimba la Kambarage mjini Shinyanga kuvaana na Mwadui FC.

Ratiba hiyo itaendelea Juni 17, kwa JKT Tanzania kuialika Yanga katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kabla ya Juni 20 wenyeji hao kuwaalika tena Singida United siku ambayo Ndanda FC nayo itakuwa mwenyeji wa Biashara United katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Kadhalika, Namungo FC itaialika Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majaliwa wakati Coastal Union ikiwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika dimba la Mkwakwani mkoani Tanga wakati huo Polisi Tanzania ikiikaribisha Lipuli FC Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Alliance katika Uwanja wao wa Kumbukumbu ya Sokoine, huku KMC ikiialika Ruvu Shooting kwenye dimba la Uhuru na Simba ikiikaribisha Mwadui FC katika Uwanja wa Taifa.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa klabu ya Simba, Patrick Rweyemamu, alisema hawezi kutolea ufafanuzi kuhusu mazoezi ya timu hiyo kwa sasa, mpaka watakapokutana na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck, kujua mikakati mipya baada ya ratiba hiyo kuelekea kukutana Ruvu Shooting Juni 14, mwaka huu.

"Siwezi kuzungumzia ratiba mpaka nitakapokutana na benchi nzima la ufundi, huenda programu ikabadilika ndio naenda kukutana na kocha sasa hivi (jana mchana) kwa leo vuta subira," alisema Patrick.

Meneja huyo alisema wachezaji wanaendelea vizuri na mazoezi na kudai morali ya kila mchezaji ipo vizuri huku akieleza kuwa anashukuru tangu waanze mazoezi hawajapata mchezaji mgonjwa hata mmoja.

"Wachezaji wanaendelea vizuri hatuna majeruhi hata mmoja lengo ni kuendeleza ushindani na kubakiza kombe la ubingwa Msimbazi," alisema.

Aliwataka mashabiki wao kuendelea kuwapa sapoti kuelekea katika michezo iliyopo mbele yao.

Habari Kubwa