Sababu saba kipigo Taifa Stars

03Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu saba kipigo Taifa Stars

MDAU wa michezo,  Dk. Athumani Kihamia, ametaja sababu saba zilizosababisha timu ya Taifa Stars kupoteza michezo yote mitatu kwenye michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 inayoendelea nchini Misri.

Taifa Stars.

Dk.Kihamia amesema leo kuwa moja ya sababu ni uteuzi wa wachezaji hao haukuzingatia uhalisia kwa wale waliofanya vizuri kwenye ligi ya ndani ili wajumuishwe.

"Mfano Jonas Mkude kwenye kiungo cha kukaba, Ibrahim Ajibu kwenye pasi za mwisho alipoongoza Tanzania nzima kwenye eneo hilo," amesema.

Sababu ya pili anaitaja kuwa ni kutokuwepo kwa bodi ya ligi inayoaminika hivyo kumechangia  kubadilisha ratiba ya ligi mara kwa mara kwa misingi ya utashi au kutokuwa na weledi.

"Hali hii imesababisha kuwepo kwa msimamo wa ligi usiokuwa na uhalisia na pia kuwafanya wachezaji kutokuwa na utimamu wa mwili endelevu," amesema.

Mdau wa michezo,  Dk. Athumani Kihamia.

Dk. Kihamia ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Shirika la Soka Tanzania (TFF) anataja sababu ya tatu kuwa ni ligi kukosa wadhamini.

"Hii imesababisha kutokuwepo mazingira sawa miongoni mwa washindani ambao ni vilabu, matokeo yake msimamo wa ligi hauakisi hali halisi ya ubora wa timu," anafafanua.

Pia sababu ya nne anaielekeza kwa waamuzi wa ligi kuu kuwa baadhi yao  wameonekana kuzibeba baadhi ya timu na kuziangamiza nyingine.

"Wakati haya yakiendelea  bodi ya ligi imekuwa  ikifumba macho na masikio ya wadau wake wakuu wanapolalamika na kujikita zaidi kwenye kupangua ratiba bila ulazima na bila kuangalia athari za kiuchumi na kisaikolojia kwa timu," amesema.

Dk. Kihamia anataja sababu ya tano kuwa ni Waandishi walitumia kalamu zao kuipamba Taifa stars kwa sifa ambazo hawajazifikia.

"Sababu nyingine ni uongozi wa timu ya Taifa Stars unatakiwa uwe na mchanganyiko ambao unabeba taswira ya Taifa badala ya uliopo sasa ambao unaonesha taswira ya wasanii na viongozi wachache tena waliopo Dar es Salaam," amesema.

Dk. Kihamia anasema ni vyema TFF ikaweka nguvu kubwa kwa vijana U23, U20, U17, na kurejeshwa kwa mashindano ya mikoa ambako kutaleta hamasa kubwa na kupata wachezaji wenye vipaji kwa njia rahisi.

"Wakati huo huo serikali nayo iimarishe mashindano ya shule za msingi na sekondari.

Katika michuano hiyo, Taifa Stars imepoteza mechi zote tatunza kundi C, baada ya kipigo mabao 2-0 dhidi ya Senegal kisha kuchapwa 3-0 dhidi ya Harambee ya Kenya na kuhitimisha kwa kulala 3-0 dhidi ya Algeria.

Wachezaji wa Taifa Stars wanatarajia kurejea nchini kesho wakitokea Misri tayari kuanza maandalizi ya kuwania  kufuzu maashindano ya wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani barani Afrika CHAN) dhidi ya Sudan.

Habari Kubwa