Sababu Emery kuteseka Arsenal

11Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Sababu Emery kuteseka Arsenal

TANGU alipojiunga na Arsenal kipindi cha majira ya joto mwaka 2018, Unai Emery amefurahia mwanzo wa msimu mpya, akicheza mechi 22 bila kufungwa.

Unai Emery.

Hata hivyo, haraka mambo yakageuka. Kutofungwa mechi 22 kulimalizwa na Southampton na kushuka kwa kiwango chao kukaanzia hapo kwenye dimba la St Mary. Katika kuongeza machungu zaidi wakampoteza mchezaji wao muhimu, Hector Bellerin aliyeumia misuli ya nyama za paja na akakaa nje karibia wiki nne.

Na tangu hapo, Arsenal haijawa kwenye kiwango kizuri cha kuvutia. Ingawa ni msimu wake wa kwanza Emery hapo Arsenal, lakini kuna mambo yanachangia timu hiyo kufanya vibaya.

Makala haya yanakuchambulia kwa nini Emery anapata tabu sana na Arsenal yake katika msimu wake wa kwanza kuinoa...

 

4. Majeruhi

Kama kuna sababu yoyote kubwa ya kushuka kwa kiwango cha Arsenal ni kuumia kwa wachezaji wao muhimu. Unai Emery aliwasajili wachezaji watano wakati alipojiunga na Arsenal, wanne kati yao ni wa daraja la juu kabisa. Wachezaji kama Lucas Torreira, Matteo Guendouzi, Bernd Leno na Sokratis wamekuwa nyota wa kiwango cha juu.

Hata hivyo, kukosa ubora wa kikosi cha Arsenal pengine kunaweza kuwagharibu kwa msimu wote, huku nafasi yao ya kumaliza kwenye nne bora inaweza isiwapo. Arsenal wamempoteza Rob Holding, Hector Bellerin, na Danny Welbeck kwa kipindi kirefu cha msimu kutokana na majeraha. Wachezaji hao walionekana kuwa na matumaini makubwa kwa Emery, lakini kuumia kwao kunapoteza matumaini hayo. Bellerin na Holding walikuwa wachezaji nguzo na muhimu mno kwa mbinu za Emery.

Katika mechi zake dhidi ya Manchester City, Arsenal walionekana kama wangeweza kupigana pale katika Uwanja wa Etihad. Lakini wiki moja kabla ya mchezo huo wachezaji kama Mkhitaryan na Sokratis waliumia. Beki wa kulia, Maitland Niles na kiungo wa kati Granit Xhaka hawakuwapo kwenye mchezo huo dhidi ya City kutokana na kuwa majeruhi.

Na hilo likamlazimisha Emery kucheza mchezo wa kujilinda, na walikuwa kwenye nafasi ya kufungwa mabao mengi zaidi kama walipokutana na kichapo cha 5-1 kutoka kwa Liverpool pale Anfield Januari mwaka huu.

 

3. Kukosa sapoti ya bodi  ya Arsenal

Mmiliki wa Arsenal, Stan Kroenke ameripotiwa kwamba hawekezi faida yoyote kwa klabu yake, licha ya kuwa na thamani ya pauni bilioni tano.

Arsenal, kuwa nafasi ya saba kwenye orodha ya klabu zenye thamani kubwa zaidi duniani, ilitoa matarajia kwa mashabiki wake kwamba bodi itampa nafasi Emery kusajili beki wa muda mfupi kwa ajili ya kuziba pengo la Holding, na kusajili winga kwa ajili ya Mkhitaryan na viungo wa kati kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji kama Torreira,  Guendouzi na Xhaka ambao kuna wakati wanatakiwa kupumzika.

Lakini badala yake, Emery aliripotiwa akidai kwamba Arsenal wanaweza kusajili wachezaji wa mkopo tu kwa kipindi cha dirisha dogo la usajili, kwamba hawakua na fedha ya kufanya usajili mkubwa. Hili liliwaacha mashabiki kukasirishwa. Na hawakuwa na la kufanya zaidi ya kukubaliana na hali halisi.

Arsenal imefanya usajili mmoja tu wa Denis Suarez kutoka Barcelona. Licha ya kuwa na matatizo kwenye safu ya ulinzi, bado haijawa na mpango wowote wa kumpa fedha Emery ili afanye usajili.

 

2. Hana kikosi kipana

Pale Manchester City, kama ingetokea Laporte na John Stones wamepatwa na majeraha, Pep alikuwa na mabeki wengine wawili wa daraja la juu, Kompany na Otamendi. Kama Mohammad Salah na Sadio Mane wakipata majeraha, Klopp ana Shaqiri na Daniel Sturridge ambao watachukua majukumu yao.

Hivyo hivyo kwa upande wa Chelsea kama Eden Hazard atakuwa majeruhi Pedro, Willian, Barkley au Loftus Cheek wanaweza kuziba pengo lake. Lakini kwa Arsenal ni ngumu.

Majeruhi mmoja, Rob Holding yameifanya safu ya ulinzi ya Arsenal kupwaya. Mustafi hajawa vizuri zaidi kucheza kwa ubora na Sokratis bado hajawa katika ubora. Majeruhi Mkhitaryan na kushuka kwa kiwango kwa Mesut Ozil yameigharimu Arsenal.

Emery hana mbadala wa wachezaji wengi ambao wapo kwenye kiwango bora kuweza kuibeba timu. Arsenal ilikuwa na nafasi ya kukiimarisha kikosi chao, lakini bodi ikashindwa kutoa fedha, hivyo hawana kikosi kipana cha kuweza kupambana msimu wote na katika mashindano yote.

 

1. Mabeki wenye viwango duni

Arsenal wameruhusu mabao mengi zaidi kati ya timu sita za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakifungwa mara 36, moja zaidi ya Manchester United. Wamekuwa na matatizo makubwa kwenye safu yao ya ulinzi kutokana na mabeki wake wengi kuumia.

Mabeki ambao wametakiwa kuchukua nafasi ya majeruhi hawapo kwenye ubora unaotakiwa. Huku wakiwa hawajaongezewa nguvu yoyote dirisha la Januari, Emery ameshindwa kuwa na wachezaji mbadala.

Huku hali ikionekana mabeki hao kuchelewa kurudi dimbani, maana yake ni kwamba uwezekano wa Arsenal kumaliza nne-bora na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ni finyu mno.

Habari Kubwa