Sababu Mazembe kuachana na Ajibu

28May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Sababu Mazembe kuachana na Ajibu

IKIWA ni siku chache zimepita baada ya Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuonyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu, imefahamika kwamba mchakato huo umesitishwa na sababu kuanikwa.

Ibrahim Ajibu

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinameeleza kuwa TP Mazembe wamesitisha nia yao baada ya kushindwa kufikia makubaliano binafsi na mshambuliaji huyo ambaye mkataba wake na Yanga unatarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu.

Chanzo chetu kimeeleza kuwa TP Mazembe wamekumbana na ugumu huo baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba Ajibu alishaingia makubaliano ya awali na Simba, hivyo kama vigogo hao wa Congo watamhitaji wanatakiwa wafanye kwanza mazungumzo na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Mazembe walikuwa tayari kumsajili Ajibu kama mchezaji huru baada ya kuwa na uhakika kuwa Yanga bado hawajamsajili, ila haya yaliyokuwa chini ya pazia, yamewafanya wabadilishe uamuzi wao," kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, bado amekataa kusema lolote kuhusiana na usajili wa Ajibu na kiungo wa Gor Mahia Mkenya Francis Kahata ambaye tayari ameshawaaga wachezaji wenzake wa kikosi hicho cha mabingwa wa Ligi Kuu Kenya.

"Kahata yeye amemaliza mkataba wake na Gor Mahia ndio maana ameamua kuwaaga wachezaji wenzake, kuhusu kutua Simba mimi sijui, nasema subirini kwanza, naona wenzetu (Yanga) wameanza moto na usajili, " alisema Magori.

Msimu uliopita, Simba ilifanikiwa kumsajili Meddie Kagere kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake Gor Mahia na mwisho wa msimu aliwaaga wenzake pamoja na viongozi kuwa anarejea kwao Rwanda, lakini siku iliyofuata alitua jijini na kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa