Sadney, Balinya waishtua Yanga

25Mar 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Sadney, Balinya waishtua Yanga
  • ***Yasema haitafanya tena makosa, Eymael aachiwa kazi ya usajili amalize mwenyewe...

BAADA ya 'kubugi stepu' katika dirisha kubwa la usajili lililopita, uongozi wa klabu ya Yanga umeamua kuliacha jukumu hilo kwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Luc Eymael ili kutafuta nyota anaoamini wanaweza kumsaidia kujenga kikosi imara msimu ujao.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, picha mtandao

Uongozi huo umeamua kufikia hatua hiyo baada ya kukiri mwanzoni mwa msimu huu ulisajili wachezaji ambao hawakuwa msaada kwa timu yao na hatimaye kuishia kuvunja mikataba na kuondoka katikati msimu.

Wachezaji ambao wanaonekana kuishtua Yanga na kuifanya kutotaka kurudia makosa ni washambuliaji Mganda Juma Balinya ambaye alikuwa mfungaji bora nchini Uganda na Mnamibia Sadney Urikhob, waliokuwa gumzo wakati wa usajili wao, lakini wakashindwa kuonyesha cheche Ligi Kuu Bara na kuishia kuvunja mikataba yao na kuondoka.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema jukumu kubwa la usajili kwa sasa liko chini cha Eymael ambaye anafahamu wachezaji wazuri wa kuweza kusaidia timu yao.

Alisema hatua hiyo ni kutokana na uongozi kutotaka kurudia makosa ya nyuma ya kusajili wachezaji ambao hawakufikia malengo waliyotarajia.

"Hatuwezi kurudia makosa, Eymael anafanya majukumu yake na anapomuona mchezaji ambaye atakuja kusaidia timu, viongozi wanaenda kumalizana na mchezaji au klabu kama bado ana mkataba nayo," alisema Mwakalebela.

Alisema Luc amepewa jukumu hilo kwa kuwa amekuwa akifanya kazi kwa ukaribu na wachezaji wengi na Kamati ya Usajili ya Yanga haina mpango wa kumuingilia kwenye majukumu yake.

Yanga tayari imekata tamaa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ambao inaukosa kwa msimu wa tatu mfululizo na kushuhudia watani zao, Simba wakilibeba taji hilo linalotoa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hadi sasa Simba ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 71 baada ya mechi 28, wakati Yanga iliyopo mchezo mmoja nyuma ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 51, tatu nyuma ya Azam FC katika nafasi ya pili.

Ligi hiyo kwa sasa imesimama kwa kipindi cha mwezi mmoja kutii agizo la serikali la kuepuka mikusanyiko ya watu ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya corona vinavyoendelea kupuputisha uhai wa maelfu ya watu duniani.

Katika mapumziko hayo, klabu zimekuwa zikiyatumia 'kurusha ndoana' zao huku na kule kwa kuanza kufanya mazungumzo na wachezaji inaotaka kuwasajili katika dirisha lijalo.

Habari Kubwa