Safari ya Yanga majaribu kibao

13Feb 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Safari ya Yanga majaribu kibao

MSAFARA wa klabu ya Yanga kwenda Mauritius kwa ajili ya mchezo wao wa leo wa Klabu bingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ulijikuta katika wakati mgumu baada ya kukwama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kwa zaidi ya masaa tisa.

WACHEZAJI WA TIMU YA YANGA

Kikosi cha Yanga kikiwa na wachezaji 21 na viongozi saba, awali walitakiwa kuondoka nchini alfajiri ya kuamkia jana na ndege ya Shirika la ndege Tanzania (ATCL), lakini walishindwa kuondoka kwa muda huo kutokana na ndege waliyokuwa wasafarie kupata hitilafu kabla ya aijaondoka, hivyo kukwama uwanjani kwa muda mrefu.

Taarifa za baadaye zilidai kuwa hadi saa 10.30 jioni timu hiyo ilikuwa bado kuondoka uwanjani hapo.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Salehe aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kupewa taarifa za hitilafu hiyo, walilazimika kutatafuta ndege nyingine iliyochelewa kuondoka.

"Tuliamu kurudi klabu na muda huu (saa 7:24 jana mchana) tunakwenda uwanja wa ndege tayari kuondoka," alisema Salehe.

Alisema kuwa walitarajia kufika Mauritius jana saa 2:20 usiku na leo wataingia uwanjani kupambana na wenyeji wao.

Awali, akizungumzia mchezo wao dhidi ya Cercle de Joachim, Kocha Hans van der Pluijm alisema wanakwenda kwenye mchezo huo kupambana na kupata matokeo mazuri.

Alisema wataingia uwanjani na kucheza soka la kushambulia zaidi, huku wakiwa na nidhamu ya kujilinda ili kutowaruhusu wenyejin wao kupata goli.

"Tutacheza soka letu la kasi na nataka timu ishambulie muda wote, tutajitahidi kuwabana wapinzani wetu wasipate goli nyumbanio," alisema Pluijm.

Yanga imeondoka na kikosi kizima na baada ya mchezo watakwenda Zanzibar kujiandaa na mechi dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Februari 20.

Habari Kubwa