Samata katika mtihani mzito

10Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Samata katika mtihani mzito

BAADA ya kucheza kwa dakika 24 akitokea benchi Jumapili wakati KRC Genk ikifungwa 1-0 ugenini dhidi ya Gent, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, nahodha wa Tanzania, Mbwana Samata, Jumamosi anarudi kazini.

mbwana samatta

Samata aliyeingia dakika ya 66 Uwanja wa Ghelamco-Arena mjini Gent kuchukua nafasi ya Nikolaos Karelis, anatarajiwa kuiongoza timu yake katika mchezo mwingine wa Ligi ya Ubelgiji Jumamosi wiki hii dhidi ya Waasland-Beveren kwenye Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.

Baada ya hapo, Samata na wenzake waterejea kambini kujiandaa kwa mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kwenda hatua ya makundi ya Europa League dhidi ya Lokomotiva Zagreb Alhamisi Agosti 18, mwaka huu, ambao utapigwa Uwanja wa Kranjceviceva mjini Zagreb, Croatia.

Mchezo wa marudiano utafanyika Alhamisi ya Agosti 25 katika Uwanja wa Luminus Arena, Genk na kina Samata wakifuzu mtihani huo, wataingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi, ambako watakutana na vigogo mbalimbali wa Ulaya, wakiwamo Manchester City ya England.

Ikumbukwe Samatta alijiunga na Genk kwa dau la Euro 800,000 Januari mwaka huu akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe ya DRC huku pia akiwa bora mfungaji wa michuano hiyo na pia kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora anayecheza Afrika.

Habari Kubwa