Samatta afunguka Misri imewajenga

15Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Samatta afunguka Misri imewajenga

WAKATI Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Emmanuel Amunike, amesema kuwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri (Mafarao) ulikuwa ni muhimu kwa kikosi chake, kwa sababu kiufundi bado kinaendelea kuimarika, nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta, amesema mechi hiyo imesaidia kuwajenga.

Nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta (katikati), akijaribu kuondoka na mpira katika mechi ya kirafiki dhidi ya Misri iliyochezwa juzi usiku mjini Alexabdria. Stars ililala bao 1-0. PICHA: TFF

Taifa Stars ambayo ilimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza bila ya kuruhusu goli, ilipoteza mchezo huo wa kirafiki uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria kwa kufungwa bao 1-0.

Akizungumza na gazeti hili jana, Amunike, alisema kuwa mchezo huo umemsaidia kufahamu makosa ya wachezaji wake na hivyo atayafanyia kazi kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika hapo wiki ijayo.

Amunike alisema kwamba kujipima na timu kubwa ni jambo jema kwa sababu kwa upande wake anapata faida ya kujitathmini na kurekebisha pale penye udhaifu katika kikosi chake ambacho kina wachezaji wengi wanaocheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara tofauti na ilivyokuwa kwa wapinzani wao.

"Ilikuwa ni nafasi muhimu sana kucheza na Misri, ni timu kubwa sana barani Afrika ambayo ina wachezaji wanaocheza Ulaya na wenye uzoefu, imenisaidia kujua ninapotakiwa kurekebisha, katika mpira hapa tumefanikiwa zaidi, tutakuwa imara kuelekea michuano hii ya Afrika," alisema Amunike.

Naye nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, alisema kuwa wamefurahi kujipima na timu kubwa na hapo ndio wakati mzuri wa benchi la ufundi kufahamu upungufu wa kikosi na kujipanga kuufanyia kazi.

"Wana timu nzuri, wako imara, ni moja ya timu bora barani Afrika, ndio maana ya kucheza mechi za kirafiki, tutajua wapi tumekosea ili tuweze kujirekebisha, tunafahamu tutacheza mechi ngumu katika makundi na mechi hii itatusaidia kujitambua na kurekebisha pale tulipokosea," alisema Samatta.

Hata hivyo, katika mchezo huo wa kirafiki, wenyeji Misri hawakuwachezesha nyota wake kadhaa akiwamo mshambuliaji wa Liverpool ya England, Mohammed Salah ambaye alikuwa benchi na kuonekana kufurahi wakati mechi hiyo ikiendelea.

Stars itashuka tena dimbani kesho katika mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya wenzao wa Zimbabwe katika mwendelezo wa kukiimarisha kikosi hicho.

Habari Kubwa