Samatta aing'arisha Genk Europa

11Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Samatta aing'arisha Genk Europa

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayeichezea KRC Genk ameendelea kung'ara baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa magoli 5-2 kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora wa mashindano ya Ligi ya UEFA Europa.

Mbwana Samatta.

Katika mchezo huo uliofika juzi usiku kwenye Uwanja wa Ghelamco- Arena mjini Gent, nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania, Samatta alifunga mabao katika dakika ya 41 na 72.

Magoli mengine ya timu hiyo yalifungwa na kiungo kutoka Ukraine, Ruslan Malinovskiy katika dakika ya 21, mabeki Mgambia Omar Colley katika dakika ya 33 na Jere Uronen dakika ya 45.

Mabao ya wenyeji yalifungwa na mshambuliaji kutoka Nigeria, Samuel Kalu Ojim katika dakika ya 27 na Kalifa Coulibaly ambaye ni raia wa Mali katika dakika ya 61.

Ushindi huo unaifanya Genk kuwa katika mazingira ya kusonga mbele kwa kuhitaji sare au ushindi wowote katika mechi ya marudiano itakayofanyika nyumbani kwao.

Samatta jana amefikisha mabao 16 katika mechi 47 alizoichezea Genk tangu asajiliwe Januari mwaka jana kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kati ya mechi hizo 47, michezo 18 Samatta alicheza msimu uliopita na 29 msimu huu na kati ya hizo, ni michezo 28 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na 18 msimu huu.

Mechi 19 kati ya hizo alitokea benchi, nane msimu uliopita na 11 msimu huu, wakati 11 hakumaliza baada ya kutolewa, sita msimu uliopita na tisa msimu huu na katika mabao hayo 16, 10 amefunga msimu huu na sita msimu uliopita.

Habari Kubwa