Samatta amulikwa kila kona Ligi Kuu England

28May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Samatta amulikwa kila kona Ligi Kuu England

BAADA ya kung'ara kwa kuipa timu yake ya KRC Genk ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza A nchini Ubelgiji, mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, nyota yake sasa inang'ara vilivyo Klabu za Ligi Kuu England (EPL), imeelezwa.

Mbwana Samatta.

Tayari Samatta, ameweka wazi kwamba kuna klabu nyingi za EPL zimeonyesha nia ya kuipata huduma yake kwa msimu ujao.

Alisema: “Siwezi kuzitaja kwa sasa, ila si England tu bali kuna klabu nyingine mbili kutoka Hispania ambazo zimekuwa zikinihitaji, lakini ndoto zangu ni kucheza katika Ligi Kuu ya England.

“Katika soka huwezi kujua nini kitatokea, naweza kuondoka mwishoni mwa msimu huu, kuna klabu ambayo imekuwa ikiwasiliana sana na wakala wangu.”

Hii si mara ya kwanza kuwapo kwa tetesi za Samatta kutakiwa EPL, kwa kuwa wakati wa usajili wa dirisha dogo, Januari mwaka huu, Klabu ya Cardiff ambayo sasa imeshuka daraja, ilidaiwa kutoa ofa kwa KRC Genk kabla ya mchakato huo kukubwa kukamilika.

Ingawa Samatta, 26, hakuwa tayari kutaja klabu zinazohitaji saini yake, tetesi zinaeleza kuwa Everton, West Ham na Burnley ni miongoni mwa zinazohusishwa na huduma yake.

Akiwa na mabao 23 kwenye ligi hiyo msimu huu na tisa katika michuano ya Europa League, Samatta alikuwa lulu kwa mashabiki wa timu hiyo wakati wakihitimisha msimu na kukabidhiwa ubingwa wao msimu huu.

“Genk haijacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu mwaka 2011 enzi za kina (Kevin) De Bruyne, najua wanataka niichezee msimu ujao ila Ligi Kuu ya England ina heshima yake, ni ligi ambayo tayari imepiga hatua kubwa sana ukilinganisha na Ligi Kuu ya Ubelgiji. Ni ligi ambayo inapendwa na watu wengi duniani, ligi inayoonekana sehemu kubwa duniani, ipo mbali vitu vingi.”

Habari Kubwa