Samatta asema hakuna "kufeli"

23Mar 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Samatta asema hakuna "kufeli"
  • ***Ni katika mchezo dhidi ya Uganda utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa...

NAHODHA wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta, amewataka Watanzania kutokuwa na wasiwasi na kikosi chao kuelekea mchezo dhidi ya Uganda (Cranes) utakaofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 12:00 jioni kwa sababu wamejipanga kutowaangusha.

Wachezaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) wakifanya mazoezi kujiandaa kuikaribisha Uganda katika mechi ya Kundi L itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. PICHA: SOMOE NG'ITU

Taifa Stars inanolewa na Mnigeria, Emmanuel Amunike, inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu Fainali za Afrika zitakazofanyika Juni mwaka huu nchini Misri.

Akizungumza na gazeti hili jana, Samatta alisema kuwa timu hiyo imejipandaa vema kuwakabili Uganda na kila mchezaji ana morali ya hali ya juu ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi L.

Samatta alisema kuwa watakuwa makini zaidi katika mechi hiyo ili kuwafanya wageni hao ambao wameshafuzu kutotawala mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Gabon.

"Tumepata maandalizi mazuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Uganda, tunaahidi umakini wa hali ya juu kuelekea mchezo dhidi ya Uganda utakaochezwa Jumapili," alisema nahodha huyo ambaye anacheza katika klabu ya KCR Genk ya Ubelgiji.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ammy Ninje, amesema kuwa kikosi cha timu hiyo kimekamilika kutokana na wachezaji wote walioitwa kuwasili.

Ninje alisema kuwa ili Stars iweze kushinda mchezo huo kila mchezaji atakayepata nafasi atatakiwa kutimiza jukumu lake kikamilifu.
"Tuna kikosi kizuri, ila kila mchezaji anatakiwa kufahamu anafanyanini anapokuwa na mpira na vile vile afanye nini pale anapopoteza mpira, hapo tutakuwa kwenye nafasi nzuri, na vile vile kutumia vema nafasi tutakazozitengeneza," alisema Ninje.

Taifa Stars itawakaribisha Uganda ambayo baadhi ya nyota wake akiwamo mshambuliaji, Emmanuel Okwi wa Simba wakiwa na kumbukumbu ya sare ya bila kufungana walipokutana katika mchezo wa kwanza uliochezwa Septemba 9, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Mandela (zamani Namboole) jijini Kampala.

Uganda yenye pointi 13 ndio inaongoza kundi hilo ikifuatiwa na Lesotho yenye pointi tano sawa na Taifa Stars, huku Cape Verde yenye pointi nne ambayo leo itakuwa nyumbani inaburuza mkia.

Habari Kubwa