Samatta, Coca-Cola kuibua vipaji nchini

14Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Samatta, Coca-Cola kuibua vipaji nchini

Kampuni ya Coca-Cola Tanzania imeingia makubaliano ya kumtumia nahodha wa timu ya Taifa, 'Taifa Stars' na mshambuliaji wa Klabu ya Aston Villa ya Ligi Kuu England, Mbwana Samatta katika kampeni zake ili kuwahamasisha Watanzania kufikia ndoto zao.

Nahodha wa Taifa Stars na mshambuliaji wa Klabu ya Aston Villa ya Ligi Kuu England, Mbwana Samatta ambaye ameingia makubaliano na Kampuni ya Coca-Cola Tanzania ya kuitangaza chapa ya kampuni hiyo katika kampeni zake ili kuwahamasisha Watanzania kufikia ndoto zao. PICHA: COCA-COLA

Kwa pamoja, Samatta na Coca-Cola watatumia muungano huo kuwaburudisha na kuwahamasisha Watanzania kufanya kilicho bora ili kuzifikia ndoto zao kimichezo na malengo mbalimbali ya kijamii kwa kupitia kliniki mbalimbali zitakazoandaliwa na kampuni hiyo ya vinywaji baridi.

“Tangu nilipokuwa mdogo, kila wakati kulikuwa na kitu cha tofauti kuhusu Kampuni ya Coca-Cola. Kwa njia moja, ninahisi ni kama nimeijua Coca-Cola katika maisha yangu yote na ninatambua mashabiki wangu wengi nchini Tanzania na duniani kote wanahisi vivyo hivyo,” alisema Mbwana Samatta wakati wa kutangaza ushirikiano huo.

"Ushirikiano huu na Coca-Cola kiukweli ni wa kipekee na wa aina yake, ni zaidi ya kufanya kazi na kampuni inayoongoza kwa utengenezaji wa vinywaji baridi duniani, na ni fursa kuwa sehemu ya kitu kinachougusa ulimwengu."

Aidha, ushirikiano huo umetokana na matarajio na maono ya pamoja ya Samatta na Coca-Cola kutengeneza thamani na kuleta utofauti katika jamii huku ukikusudia kuileta kampuni hiyo ijulikanayo duniani kote 'karibu na nyumbani' kwa kuiunganisha chapa yake ya na nahodha huyo wa Taifa Stars.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Chapa ya Coca-Cola Tanzania, Kabula Nshimo, alisema matakwa ya Samatta kuhamasisha, kuunganisha na kuwainua hasa vijana, ni dhihirisho la maadili ya chapa ya Coca-Cola.

"Yeye ni mfano wa kuigwa hapa nchini, anapeperusha bendera ya Tanzania vilivyo ulimwenguni, Ukiangalia historia yake alipotoka kwenye fani hii ya soka na alipofikia, kiukweli inawapa hamasa Watanzania hasa vijana kufuata ndoto zao,” alisema Nshimo.

Kampuni ya Coca-Cola imekuwa na historia ndefu ya kuunga mkono michezo, hasa mpira wa miguu katika ngazi zote kuanzia ngazi ya shina, kupitia mashindano yake ya COPA Coca-Cola.

Kwa miaka mingi mashindano haya yametengeneza fursa kwa wachezaji wengi wenye vipaji vya kipekee, kutambuliwa, kuajiriwa na kujiunga na timu ya Taifa ya chini ya miaka 20 ya Tanzania. Mmoja wa wachezaji hao Samatta ambaye alipata bahati ya kushiriki mashindano ya kwanza kabisa ya COPA Coca-Cola nchini Tanzania mwaka 2006 akiwa na timu ya Kimbangulile ya Temeke jijini Dar es Salaam.

"Kama Mtanzania ambaye ni kinara wa Soka katika anga la kimataifa, Samatta anawahimiza vijana wengi kutouchukulia mpira kama mchezo wa kujifurahisha tu, bali kama ajira, na muhimu ni kwamba wanaweza kuzifikia ndoto zao kwa urahisi, kama yeye alivyoweza.

"Kwa kuongezea tu, ni kuwa kupitia kliniki za mpira wa miguu ambazo tutakuwa tunaziandaa, tutaweza kujihusisha na kuwahamasisha vijana wengi zaidi, hii ikiwa sambamba na maono ya Kampuni ya Coca-Cola ya kuburudisha ulimwengu na kuacha alama," alisema Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Kampuni ya Coca-Cola Afrika Mashariki na Kati, Nelly Wainaina.

Alisema Kampuni ya Coca-Cola itaendelea kukuza vipaji vya vijana kupitia ushirika huo na kuamsha matumaini kwa wachezaji chipukizi wa mpira wa miguu kote nchini, huku akiwataka wadau wa michezo nchini kutegemee mengi zaidi kutoka katika muungano huo.

Habari Kubwa