Samatta kupewa mtaa D'Salaam

04Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Samatta kupewa mtaa D'Salaam

MSHAMBULIAJI wa KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji na nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta, anatarajiwa kupewa mtaa hapa jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

MSHAMBULIAJI wa KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji na nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta.

Uamuzi wa Samatta kupewa mtaa unatokana na mafanikio mbalimbali ambayo ameyapata mshambuliaji huyo ambaye msimu ujao atashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Akizungumza jana jijini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema maandalizi ya kumpa mtaa yako katika hatua za mwisho na itakuwa ni kwenye barabara ya lami.

Makonda alisema kuwa wanaamini uamuzi huo ni sehemu ya kumuenzi mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na African Lyon ambaye pia anatumika kama balozi wa utalii kwa kuitangaza nchi kimataifa.

"Ninatambua kutokana na kazi yake aliyoifanya huko, amefanikiwa kufanya mambo makubwa, tutamkabidhi rasmi mtaa ambao barabara yake itakuwa na lami safi, taa, hii itafanya aendelee kukumbukwa wakati wote," alisema Makonda.

Alieleza kuwa makabidhiano ya mtaa huo yatafanyika kabla ya kikosi cha Taifa Stars hakijasafiri kuelekea Misri kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) ambazo zitaanza kuchezwa baadaye mwezi huu.

Aliongeza kuwa serikali imejipanga kuwaenzi wanamichezo wote watakaopeperusha vema bendera ya Tanzania na watakaokuwa na maadili safi, kwa sababu hii inasaidia kuwajenga wanamichezo wanaochipukia.

Pia, Makonda alisema kuwa serikali haitasita kutoa adhabu kwa wanamichezo ambao watafanya vibaya na kuchafua jina la nchi.

Wakati huo huo, Makonda, alisema kwa kushirikiana na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E), wako katika hatua nzuri za kujenga uwanja wa michezo pamoja na kujenga ukumbi wa kisasa kwenye eneo la Tanganyika Packers, Kawe.

Habari Kubwa