Sancho: Ndoto yangu imetimia kwa Man U

26Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Sancho: Ndoto yangu imetimia kwa Man U
  • …Aishukuru Dortmund kumpa nafasi na alijua atarudi England kwa…

WINGA wa England, Jadon Sancho amesema kwamba, kujiunga na Manchester United ni ndoto iliyotimia baada ya kukamilisha uhamisho kutoka klabu ya Borussia Dortmund kwa dau la pauni milioni 73, mapema juzi.

Sancho ndiye mchezaji wa pili wa England mwenye thamani ya juu baada ya mchezaji mwenza wa United, Harry Maguire na amesaini mkataba wa miaka mitano kuichezea klabu hiyo.

“Naishukuru Dortmund kwa kunipatia fursa ya kucheza katika kikosi cha kwanza, ingawa nilijua kwamba nitarudi England,” alisema Sancho mwenye umri wa miaka 21.

“Fursa ya kujiunga na Manchester United ni ndoto iliyotimia na sasa nasubiri kuonyesha umahiri wangu katika Ligi Kuu ya England, EPL.”

“Hiki ni kikosi kichanga na najua, pamoja tunaweza kujenga kitu maalum ili kuleta ufanisi ambao mashabiki wanahitaji.”
United waliafikia makubaliano ya kumsajili Sancho Julai Mosi, mwaka huu na kandarasi yake ya miaka mitano na klabu hiyo ina kifungu cha kuongezewa miezi mingine 12.

Ukamilishaji wa makubaliano hayo unasitisha uwindaji wa kumsajili mchezaji huyo. Walitarajiwa kumsajili msimu uliokwisha lakini wakatofautiana kuhusu dau la uhamisho wake.

Sancho alifunga mabao 50 na kutoa usaidizi wa magoli 57 katika mechi 137 alizochezea Dortmund.

Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer amesema kwamba Old Trafford itampatia Sancho fursa anayohitaji kuonyesha kipaji chake.

“Jadon ni aina ya mchezaji ambaye nilipenda kumleta katika klabu hii – ni mshambuliaji anayeingiliana na utamaduni wa Manchester United,” alisema Solskjaer akiiambia tovuti ya klabu hiyo.

“Atakuwa kiungo muhimu wa kikosi changu kwa miaka kadhaa ijayo na tunatarajia kwamba atang’ara.

“Mabao yake na rekodi yake ya usaidizi ni ya kipekee na pia atatuongezea kasi katika mchezo wetu, umahiri na ubunifu katika timu.”

Kurudi kwa Sancho katika Ligi ya England kunajiri baada ya kuisaidia timu ya taifa kufuzu katika fainali ya kombe la Euro 2020, ambapo walifungwa na Italia kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Mchezaji huyo wa zamani wa kikosi cha vijana cha timu ya Manchester City pamoja na Bukayo Saka na Marcus Rashford walikabiliwa na ubaguzi wa rangi katika mitandao ya kijamii baada ya kushindwa kufunga penalti muhimu walizopewa.