Sarpong akiri Ligi Kuu Bara ngumu

15Sep 2020
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Sarpong akiri Ligi Kuu Bara ngumu

LICHA ya kwamba ndiyo kwanza amecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara, mshambuliaji hatari wa Yanga, Mghana Michael Sarpong, amekiri ligi hiyo ya Tanzania ni ngumu na yenye ushindani mkali.

Mghana Michael Sarpong:PICHA NA MTANDAO

Sarpong aliifungia Yanga bao la kusawazisha wakati ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu Bara Septemba 6, mwaka huu katika Uwanja wa Mkapa.

Hata hivyo, licha ya kuhaha kutaka kuendeleza kasi yake ya kucheka na nyavu, juzi alishindwa kufua dafu mbele ya mabeki wa Mbeya City katika mchezo wao wa raundi ya pili uliopigwa Uwanja wa Mkapa na Yanga kushinda kwa bao 1-0 dakika za mwisho.

Bao hilo pekee la Yanga lilifungwa kwa kichwa na beki wa kati, Mghana Lamine Moro akiutendea haki mpira wa kona uliochongwa na kiungo Muangola Carlos Carlinhos dakika ya 86.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam, Sarpong alisema lengo lake ni kuipa mafanikio timu yake kwa kuiwezesha kushika nafasi ya juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ligi hiyo ni ngumu na yenye ushindani mkubwa.

"Ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa, kutokana na kila timu kujipanga kupata matokeo mazuri pindi inapokuwa uwanjani, ninaona jinsi timu zilivyojipanga vizuri kila moja inataka kushika nafasi ya juu," alisema Sarpong.

Kuhusu mechi hiyo ya juzi, alisema ilikuwa ngumu, lakini ameshukuru timu yake kuondoka na pointi tatu uwanjani.

Akizungumzia ushindani wa namba, Sarpong alisema ni mkubwa katika kikosi chao, lakini atazidi kujituma kwa nguvu zote kila akipata nafasi ili kujihakikishia kucheza na kuipa mafanikio timu kama alivyoahidi kipindi anatua nchini.

"Ninashukuru wachezaji wenzangu wamenionyesha ushirikiano kuanzia nilipofika sijaona tofauti yoyote, ninaahidi mashabiki wangu kufanya vizuri," alisema.

Aidha, aliwataka mashabiki na wanachama wa Yanga kuendelea kumpa sapoti ili aweze kuipa ushindi timu yake pindi watakapokutana na Kagera Sugar, Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Habari Kubwa