SBL yajipanga kuwapa furaha mashabiki Stars

08Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
SBL yajipanga kuwapa furaha mashabiki Stars

KUELEKEA mechi dhidi ya Equatorial Guinea, Mdhamini Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), kupitia kinywaji chake cha Serengeti, imesema kuwa itaendelea kuwapa raha mashabiki wa soka hapa nchini.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao (kulia), akizungumza kuhusu maandalizi ya mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Equatorial Guinea, itakayochezwa Novemba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Katikati ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Anitha Rwehumbiza na Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa, Haji Manara. PICHA: JUMANNE JUMA

Taifa Stars inatarajia kucheza mechi ya kuwania tiketi ya kufuzu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2021), dhidi ya Equatorial Guinea itakayochezwa Novemba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja Masoko wa SBL, Anitha Msangi, alisema SBL kupitia bia yake ya Serengeti, ipo bega kwa bega na Taifa Stars pamoja na mashabiki wa soka hapa nchini.

Anitha alisema, ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanafurahia mechi hiyo, SBL, imejipanga kuweka "screen" kubwa katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuonyesha mchezo huo bure huku nafasi ya kufurahia bia ya Serengeti ikitolewa pia.

“SBL kupitia bia yetu ya Serengeti tutaendelea kuwapa burudani mashabiki wa soka kwa kuhakikisha tunaiwezesha timu yetu ya Taifa inafanya vizuri, lakini kupitia bia ya Serengeti kuwafanya mashabiki wafurahie mechi pamoja na bia yao pendwa, tujitokeze kwa wingi kuishangilia timu yetu huku tukifurahia bia yetu ya Serengeti ambayo ni fahari yetu,” alisema Anitha.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kidao Wilfred, alisema timu itaingia kambini mapema wiki ijayo ili kujiandaa na mchezo huo.

Kidao alifafanua kuwa, baada ya mchezo huo, kikosi cha timu hiyo kitasafiri kuwafuata Libya katika mchezo wa pili ambayo utachezwa Novemba 19, mwaka huu, ikiwa ni siku nne tu baada ya kucheza mchezo wa kwanza.

“Tunawaomba Watanzania kwa pamoja tuungane kwa ajili ya timu yetu ya Taifa. Tujitokeze kwa wingi siku ya mechi na kuishangilia kwa nguvu zetu zote ili kuwapa hamasa wachezaji wetu waweze kufanya vizuri,” alisema Kidao.

Habari Kubwa