Selasela, Wambura kazi ipo Umakamu Rais TFF

27Jun 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe
Selasela, Wambura kazi ipo Umakamu Rais TFF

WAKATI leo ikiwa ni siku ya pili kupokea pingamizi ya wagombea wa nafasi mbalimbali ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), uchunguzi uliofanywa na gazeti hili-

Michael Wambura.

unaonyesha wagombea wawili kwenye nafasi ya Makamu wa Rais, Robert Selasela na Michael Wambura ndiyo tishio zaidi katika kiti hicho.

Wagombea hao watachuana na Geofrey Nyange 'Kaburu', Mlamu Nghambi pamoja na Mtemi Ramadhan katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 12, mwaka huu mkoani Dodoma.

Baadhi ya wadau wa soka waliliambia Nipashe kuwa kutakuwa na mchuano mkubwa kati ya Selasela na Wambura hasa kutokana na kutokuwa na makandokando yoyote.

"Mimi nafikiri kwa nafasi ya umakamu hao wawili watachuana sana kwa sababu wengine suala la kuhusishwa na timu hizi kubwa kunaweza kukawanyima nafasi, ila kikubwa nafikiri tusubiri wakati wa kampeni kusikiliza sera zao kwa sababu tunataka kiongozi mwenye uchu wa kweli wa mafanikio ya soka letu na si kujifaidisha yeye," alisema mmoja wa wadau wa soka ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Katika nafasi ya urais pamoja na kujitoa kwa Athuman Nyamlani, bado kunatarajiwa kuwapo kwa ushindani mkubwa katika kuwania nafasi hiyo ya juu TFF.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Mwanasheria Revocatus Kuuli, kesho itakamilisha kupokea pingamizi na keshokutwa itaanza kuzipitia.

Habari Kubwa