Senzo alisema hayo kufuatia Mkuu wa Idara ya Habari wa Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, kumlalamikia kwa kitendo chake cha kwenda kuonana na kocha huyo siku moja kabla ya Wekundu wa Msimbazi kuwavaa Al Ahly.
Kiongozi huyo alisema aliamua kwenda kukutana na Mosimane kwa sababu ni 'swahiba' wake kwa sababu hawajaonana kwa muda mrefu.
Katika mitandao ya kijamii zilivuja picha zinazoonyesha Senzo ambaye alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba akiwa na Mosimane ambao wote ni raia wa Afrika Kusini, wakifanya mazoezi.
"Hakukuwa na siku nyingine ambayo ningeweza kwenda kuonana naye zaidi ya Jumatatu. Nisingeweza kuonana naye siku ya Jumanne kwa sababu walikuwa na ratiba ya kusafiri," alisema Senzo.
Alisema kuwa hana kitu cha kumwambia kocha huyo ambaye yeye hakijui, na badala yake alikwenda kuonana naye kama rafiki yake, kusalimia na wakanywa naye kahawa.
"Kitu gani ambacho naweza kumwambia Mosimane ambacho yeye hajui? Kwa kifupi, nilikutana na rafiki yangu ambaye sijaonana naye muda mrefu. Nilionana naye sehemu ya wazi ambayo kila mtu anaona na nilikunywa naye kikombe cha kahawa. Lakini naelewa niko kwenye ulimwengu wa Tanzania," Senzo alisema.